UTUME KWA VIJANA 1
Sahaya G. Selvam, SDB
Hali ya Vijana wa Siku Hizi: Ukweli na Uwongo
“Vijana wa siku hizi… hatuelewani nao! Kizazi hiki kimepotea! Dunia imechafuka!” Malalamiko ya watu wazima kuhusu vijana ndiyo haya. Hata vijana wanaweza kukubali kirahisi na sentensi zifuatazo:
- Vijana wanaonekana kuwa waasi.
- Vijana wa siku hizi hawajali dini.
- Vijana hawaelewani na wazazi wao.
- Vijana wanapendelea zaidi kusoma makala za burudani, vitabu vya hadithi (riwaya) na kutazama TV na Filamu.
- Asilimia kubwa ya vijana wa mijini hawajijali, na hutumia madawa ya kulevya.
- Vijana wa siku hizi wanapenda kupiga kelele nyingi, wakorofi, na wasumbufu.
- Vijana wanatarajia kupata burudani tu kutoka kwenye vituo vya vijana.
- Vijana siku hizi wanakosa maadili na msimamo wa kidini.
- Vijana wa siku hizi hawana malengo katika maisha.
Je, mawazo haya ni kweli? Kwa kawaida tunasema “Vijana hawajali dini.” Lakini tukihesabu vijana wanaofika kanisani jumapili ya kawaida wanaweza kuwa wengi tu. Pengine tunasema, “Vijana ni walevi, wavuta bhangi…” Lakini asilimia ngapi ya vijana wako katika hali hii? Ni asilimia ndogo sana. Tunawatupia wote tabia za wachache.
Ukweli ni kwamba kila kizazi kina matatizo yake. Hata Adamu aliposikia kwamba mwanaye Kaini amemwua Abeli labda alisema, “Kizazi hiki kimeharibika.”
Matatizo ya kila kizazi ni matokeo ya matatizo ya kizazi kilichopita, kwa sababu vijana hawashuki kutoka mbinguni. Jamii imechangia kuwalea vijana wa leo na kuwafanya jinsi walivyo.
Hata hivyo matatizo ya vijana wa karne hii ni ya kipekee, ukilinganisha na yale ya kizazi kilichopita. Tupate maelezo zaidi.
Ujana ndio nini?
Kijana ndiye nani? Kigezo cha kwanza katika kuelewa ujana kinaweza kuwa umri. Lakini kuhusu kigezo cha umri tunaona kwamba kuna tofauti sana kati ya nchi na nchi, au taasisi moja na nyingine.
Taasisi/Nchi | Umri (miaka) |
Umoja wa Mataifa (UN) | 15-24 |
Umoja wa nchi za Madola (Commonwealth) | 15-29 |
Uganda | 15-19 |
Kenya | 15-30 |
Tanzania | 15-35 |
Malaysia | 15-40 |
Kiwango kipi ni sahihi? Labda utasema ni kati ya miaka 15 na 35, kwa sababu wewe ni Mtanzania! Viwango hivi vinachangia katika kuongeza matatizo kwa vijana. Vijana wenyewe na watu wazima pia hawaelewi ujana ndio nini. Hii ni mojawapo ya vyanzo vya matatizo ya vijana. Kwa mfano, kijana wa umri wa miaka 16 akimwomba baba yake aende kwenye disko, baba yake anaweza kumkatalia ruhusa akisema, “Hapana, bado wewe ni mtoto tu!” Lakini kesho yake baba yule yule anapomtuma kijana yule kwenye shughuli maalumu anaweza kumwambia, “We, mwanangu fanya kazi hii vizuri sana. Kumbuka wewe ni mtu mzima sasa.”
Aidha, tutambue kwamba jamii inayoweka kiwango cha kufikia utu uzima kuwa kikubwa (kama Tanzania au Malaysia) inawanyima vijana wao mamlaka ya uamuzi na uongozi katika jamii yao. Inaonesha hofu fulani kati ya wazee wao. Kumbe, mtu aliyefikia umri ya miaka 40 pengine hana nguvu wala mawazo mapya, ndiye atakayekubalika kuwa mtu mzima. Jamii ya aina hii haitakuwa na mageuzi, mabadiliko, au hata maendeleo.
Maelezo mengine au kigezo kingine katika kuelewa ujana ni kuwa na nguvu, ubunifu, mawazo mapya, na hamu ya kujaribu mambo mapya. Maelezo haya yanaweza kufaa, lakini tunaelewa pia kwamba wapo wazee wenye nguvu, ubunifu, mawazo mapya, na hamu ya kujaribu mambo mapya!
Kwa ujumla, ujana ni hali ya mpito, kati ya utoto na utu uzima. Kwa hiyo vijana wanatafuta hadhi ya nafsi zao. Pengine kijana anajionesha kuwa mtu mzima, hasa katika kujaribu mambo makubwa na mapya, kama kuvuta sigara au kunywa pombe. Lakini pia bado anaelekea katika tabia ya kuchezacheza kama mtoto.
Vijana wa Siku Hizi : Mabadiliko ya Ujana kimataifa
Kuelewa vijana wetu wa karne hii tunahitaji kuzingatia walau mambo mawili ya kimaumbile ambayo yamewaathiri vijana.
1. Umri wa kupevuka umewahi:
Wataalamu wanasema kwamba mwanzoni mwa karne ya ishirini (mwaka 1900), msichana mwenye afya ya wastani alifika katika hali ya kuvunja ungo (yaani, kuingia hedhini mara ya kwanza) akiwa na umri wa miaka 19. Lakini mwanzoni mwa karne ya ishirini na moja, msichana wa kawaida anaweza kuvunja ungo akiwa na miaka kati ya 12 na 14; pengine hata akiwa na miaka 10. Mabadiliko haya yameletwa na maendeleo ya lishe na huduma ya afya, hasa kati ya wakazi wa mijini. Hali hii ni kweli pia upande wa wavulana.
2. Umri wa ndoa na kutulia kikazi umechelewa:
Ingawa kwa upande mmoja umri wa kupevuka umewahi, kwa upande mwingine umri wa kuanza maisha ya mtu mzima umechelewa, yaani, umri wa ndoa na kuanza kuwajibika kijamii. Mabadiliko haya yameletwa na utaratibu wa kwenda shule na vyuo vikuu. Elimu ya vyuo inachelewesha pia umri wa kufunga ndoa na kuanza kufanya kazi ya mshahara.
Matokeo ya mabadiliko haya ni kwamba ujana wenyewe umerefuka. Mwaka 1900, yule msichana aliyebaleghe akiwa na umri wa miaka 19, pengine alikuwa ameolewa kabla yake. Kwa hiyo, huyo alikuwa hana ujana; alivuka moja kwa moja kwenda utu uzima kutoka utoto. Lakini tumwangalie msichana wa karne hii aliyevunja ungo akiwa na miaka 12 na kuolewa akiwa na miaka 25 au 28. Miaka ya mpito imeongezeka. Msichana huyu hajui namna ya kukabili hali yake ya ujana, wala mabadiliko yake ya kimaumbile.
Katika hali hii tunaweza kuelewa vizuri zaidi takwimu kadhaa zinazopatikana hapa nchini Tanzania, kama zile zifuatazo:
- Kadiri ya takwimu za Tanzania Demographic & Health Survey-1996, umri wa wastani wa ngono kwa mara ya kwanza nchini Tanzania ni umri wa miaka 16.9.
- Takwimu za TANESA-1997 zinadai kuwa mkoani Mwanza asilimia 75.8 ya wasichana wa darasa la saba walikuwa wameshafanya ngono; na kabla ya kufikia umri wa miaka 16, asilimia 80.1 walikuwa wameshafanya mapenzi. (Kuleana, Education in Tanzania, 1999, p.59)
Kwa haya yote hatuidhinishi maovu yanayotendeka na vijana, ila tunasisitiza umuhimu wa kuelewa upya namna ya kuwalea vijana. Tukiunganisha mabadiliko haya ya kimaumbile na mabadiliko mengine ya kijamii, kama vile, maendeleo ya vyombo vya mawasiliano, uchumi wa ubepari, utandawazi, uhamiaji kwenda mijini, n.k., hatuna budi tuwahurumie vijana wetu. Kuwa kijana siku hizi ni kazi!
Matatizo Makuu Matatu ya Vijana Watanzania
Baada ya kuelewa walau kidogo hali ya vijana kimataifa tujitahidi kuelewa zaidi matatizo ya kipekee ya vijana watanzania. Ningependa kutaja hasa matatizo matatu.
1. Vijana Watanzania hukosa nafasi
Vijana watanzania huwa wanakosa nafasi ya kujiendeleza – kielimu na kiajira. Wanakosa pia nafasi ya kutosha kwa ajili ya kujiburudisha, na kupata huduma za afya. Tuangalie tu takwimu kadhaa zinazohusu elimu:
Uandikishaji wa wanafunzi Shuleni
Walioingia | Walioacha | |
Shule za Msingi | 56% | 62% |
Shule za Sekondari – O level | 5.5% | 20% |
Shule za Sekondari – A level | 1.5% | n/a |
Vyuo vikuu | 0.27% | n/a |
(Kutoka, Kuleana, The State of Education in Tanzania, 1999)
Takwimu hizi zinaonesha kwamba kwa upande mmoja wanaoingia shule ni wachache, na kati yao wanaoacha shule katikati ni wengi. Wengine huacha shule kutokana na matatizo kama vile kupata mimba, kukosa karo, na kushindwa kuukabili ugumu wa masomo – ugumu huu husababishwa na pia mabadiliko ya lugha kwa ghafla katika shule za sekondari.
Hata baada ya kuhangaika kumalizia elimu vijana hawana uhakika wa ajira. Asilimia karibu 75 ya vijana waliobaki nyumbani baada ya darasa la saba wafanyeje? Serikali husema wajiajiri. Tukumbuke kwamba hali hii inaweza kuchangia vijana wenye umri chini ya miaka 18 kuajiriwa bila kupewa haki zao, ambako ni kosa la jinai la “ajira kwa watoto”. Suluhisho lingine ni kuwaingiza vijana hawa katika shule za ufundi. Hata hii ina hatari zake. Idadi ya wenye ufundi stadi ikizidi watakosa ajira pia. Na kwa kawaida wenye elimu ya msingi wanakosa ubunifu wa kujiajiri. Kujiajiri kwenyewe ni kivuli tu kama hakuna soko kwa vitu vinavyotengenezwa na mafundi.
2. Vijana wa Tanzania ni wahamiaji
Kwa vile wanakosa nafasi za kujiendeleza, vijana huhama sana kutafuta nafasi za elimu na ajira. Wale wa vijijini huhamia mijini, wale wa mijini huhamia jijini, wakiwa na matumaini kwamba watapata nafasi sehemu nyingine. Ukweli ni kwamba daima nyasi za ng’ambo huonekana kuwa kijani zaidi; na hakuna nafasi hata mijini na jijini.
Kuhama kwa wengi husababisha msongamano wa watu mijini. Wengine huishia mitaani kama “wamachinga”. Msongamano huongeza pia matatizo ya kisaikolojia na kimaadili. Uhamiaji wa vijana kwenda mijini na kurudi vijijini pia husaidia katika kusambaza VVU (Virusi vya Ukimwi).
Upande wa vikundi vya vijana katika taasisi zetu za kanisa tunaweza kuona kwamba kila miezi sita tunakuta watu wapya na vijana tuliowalea wameondoka. Kuondoka kwao kuleta uhaba wa uongozi thabiti katika kikundi, na kukatisha tamaa kwa wanakikundi.
3. Vijana wa Tanzania “wamechanganyikiwa”
Kati ya matatizo tuliyoyataja hapo juu vijana hupata kuchanganyikiwa. Wanachanganyikiwa kwa sababu daima wanapata jumbe zinazowachanganya:
- Kanisani na shuleni vijana wanafundishwa kuwa na nidhamu na msimamo mzuri wa kimaadili. Lakini wanayoyaona nyumbani kati ya wazazi wao na ndugu zao ni kinyume kabisa na waliyofundishwa..
- Wanaona na kusikia mambo ya fahari na maisha ya starehe katika vyombo vya mawasiliano. Lakini hali ya nyumbani ni ya kusikitisha sana, kwa upande wa huduma za kawaida. Maisha yao ya kila siku ni ya mahangaiko tele.
- Vijana wana nguvu, ubunifu, ndoto za ajabu. Lakini uwezo huu mkubwa huzamishwa na ukosefu wa nafasi za kujiendeleza. Wanakosa malengo ya muda mrefu, na kukata tamaa.
- Elimu ya kimagharibi inawafundisha namna ya kutumia akili zao kuelewa matukio mbalimbali ya kiasili. Pengine elimu hafifu huwapa nafasi ya kuchekea mila na desturi za kiasili, na kutupa miiko yote. Elimu halisi kwa ujumla huwapa uhuru wa aina yake. Lakini wazee wao huweza kuwabana vijana kwa kuwalazimisha katika mambo ya mila, kama vile, ukeketaji, uchawi, chanjo, n.k. Jumapili vijana wanaambiwa kanisani kwamba mambo yote ya uchawi na uganga ni dhambi, lakini kesho yake wanalazimishwa na wazazi wao wakatoliki kuwapeleka kwa wachawi.
Mambo haya ni machache tu kati ya mengi yanayowachanganya vijana wetu. Dalili za kuchanganyikiwa huonekana hasa kati ya wasichana wakati wa sala na ukimya, na katika mafungo ya kiroho.
Katika hali hii ya vijana wetu itikio la kanisa ni lipi? Kanisa linaweza kuwalea vijana namna gani? Wajibu wa wanakanisa ni upi? Ndiyo mada ya mfufulizo wa makala hizi.
(Itaendelea…)