UTUME KWA VIJANA 2
Sahaya G. Selvam, SDB
Yesu : Mfano Bora wa Utume kwa Vijana
Vijana wenyewe si matatizo, bali wanaweza kuwa na matatizo. Ni wajibu wa wanakanisa kuwasindikiza vijana na kuwasaidia ili wenyewe watatue matatizo yao. Huu ndio utume kwa vijana. Aliyetoa mfano mzuri kwa utume huu kwa vijana ni Yesu mwenyewe. Katika makala hii tutafakari jinsi Yesu mwenyewe alivyowasaidia vijana wawili, waliokuwa wamekata tamaa, kujenga matumaini na wenyewe kuwa mitume kwa vijana (wafuasi) wengine.
Tunapata mfano huu katika tukio la “Safari ya Kwenda Emau” (Lk 24:13-35)
Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu. Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia. (Lk 24: 13-14, Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa.)
Ningependa kufikiria kwamba hawa wafuasi wawili walikuwa vijana. Kadiri ya Sera ya Maendeleo ya Vijana katika nchi nyingi kama Tanzania, kijana ni mtu yeyote mwenye umri ya miaka kati ya 15 na 35. Kwa maana hii, Yesu mwenyewe alikuwa kijana. Bila shaka wafuasi wake wengi pia walikuwa wenye umri wa miaka chini ya 35.
Basi, hawa vijana wawili walikuwa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu. Injili inasisitiza kwamba walikuwa wanaondoka “siku hiyohiyo”. Siku hiyo ilikuwa siku ya ufufuko wa Bwana. Maana yake ni kwamba walikuwa hawajaamini kuwa Yesu alikuwa amefufuka. Kweli, ni wazi kuwa walikuwa wanatoroka kutoka Yerusalemu. Ndiyo maana Yesu alipowauliza “Mnazungumza nini huku mnatembea?” Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni. Chanzo cha tatizo lao kilitokana hali kwamba walikuwa hawajampokea Yesu kuwa Mwana wa Mungu; kwao Yesu alikuwa tu nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote.
Hali ya wafuasi hawa wawili inafanana na vijana wa siku hizi. Vijana wengi wamekata tamaa na kanisa; baadhi yao hawana malengo maalumu katika maisha yao; na wengine hawana matumaini na taasisi mbalimbali za jamii, kama vile, siasa, uchumi, familia, n.k. Wengi wao wanalitoroka kanisa; wamekuwa kama watalii wa kiimani, wanazungukia makanisa mbalimbali wakitafuta wokovu wa kirahisi. Wengine wanazitoroka desturi na mila za jamii zao. Hatimaye wanajikuta wamepoteza mizizi yao.
Twawezaje kuwasaidia vijana hawa? Hebu, tuangilie jinsi Yesu alivyowasaidia Kleopa na mwenzake.
Utume wa Kujenga Mahusiano
Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao. Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua. Akawauliza, “Mnazungumza nini huku mnatembea?” Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni. Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, “Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?” Naye akawajibu, “Mambo gani?” Wao wakamjibu, “Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote. Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha. Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka. Tena, wanawake wengine wa kwetu wametushtua. Walikwenda kaburini mapema asubuhi, wasiukute mwili wake. Wakarudi wakasema kwamba walitokewa na malaika waliowaambia kwamba alikuwa hai. Wengine wetu walikwenda kaburini wakashuhudia yale waliyosema hao wanawake; ila yeye hawakumwona.” (Lk 24: 15-28)
Kwanza, Yesu aliwakuta vijana wake wawili mahali walipokuwepo: njiani, wakiwa katika harakati ya kutoroka, pamoja na matatizo yao. Hali kadhalika mlezi wa vijana anatakiwa pia kuwakuta vijana wake mahali walipo: kama vile, mitaani, vijiweni, shuleni, mashambani, na hata kwenye baa. Iwapo tukijenga taasisi fulani na kuwasubiria vijana, pengine wanaweza wasije kamwe. Kanisa la leo, hasa barani Afrika linahitaji mageuzi katika kuacha mbinu yake ya “misheni” na kutumia mbinu ya “umisionari” ili habari njema iwafikie vijana wetu. Mbinu ya “misheni” ni ya zamani, ambayo inalazimika kujenga majengo na kusubiri watu na hasa vijana waje kupata huduma mbalimbali kama ile ya imani, elimu na afya. Lakini mbinu ya “umisionari” haitegemei sana majengo, bali wahudumu kama padre na katekista wawafikie watu mitaani na katika jumuiya ndogo ndogo.
Pili, Yesu alianza kuwasikiliza kabla ya kuwahubiria. Yesu wakati ule tayari alikuwa anatumia mbinu za kisasa zinazopendekezwa na saikolojia. Yeye anajifanya kuwa mjinga ili ajenge uhusiono na wafuasi wake. Hali kadhlika, kanisa halina budi lisikilize vijana wetu. Moyo wa kusikiliza hujenga mahusiano. Kusikiliza hujenga matumaini kati ya vijana. Kujenga mahusiano pia ni sehemu ya utume. Vijana wanapojisikia kwamba wanasikilizwa ndipo wanapoweza kuwasikiliza wahudumu wa kanisa. Mambo kama michezo mbalimbali na burudani yana sehemu muhimu katika utume kwa vijana, yaani kujenga mazingira ya kuwasaidia vijana kujisikia wako nyumbani.
Utume wa Uinjilishaji
Kisha Yesu akawaambia, “Mbona mu wapumbavu kiasi hicho na mioyo yenu ni mizito hivyo kusadiki yote yaliyonenwa na manabii? Je, haikumpasa Kristo kuteswa, na hivyo aingie katika utukufu wake?” Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote. (Lk 24: 25-27)
Utume kwa vijana ambao unaisha na burudani na michezo peke yake hautadumu. Mlezi anatakiwa kuwasindikiza vijana katika hatua nyingine sasa. Anapoona wakati umefika anatakiwa kutoa changamoto kwa vijana. Ndivyo Yesu anavyofanya. Kwa vile anajua kwamba amejenga uhusiano mzuri nao, anathubutu kuwaita “wapumbavu!”
Hatua ya pili katika utume kwa vijana ni uinjilishaji. Mlezi anatakiwa kutumia Maandiko Matakatifu kuwasaidia vijana ili kutambua kwamba hata kati ya matatizo na mahangaiko ya maisha yao Mungu yupo. Mungu ndiye mtawala wa historia. Mungu ana mpango wa pekee kwa kila mmoja. Maandiko Matakatifu hayakuandikwa kwa lengo la kubishana juu yake. Bali, madhumuni ya Neno la Mungu ni kutupa sisi wanadamu dira ya maisha, hasa pale tunapokata tamaa.
Utume wa Katekesi
Walipokikaribia kile kijiji walichokuwa wanakiendea, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari; lakini wao wakamsihi wakisema, “Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia.” Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao. Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao. (Lk 24: 28-31)
Kwa kweli kama mlezi amejenga uhusiano mzuri na vijana, tena amewagusa upande wa imani, hasa kwa kutumia Maandiko Matakatifu vijana wanaweza kusema, “Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa.” Ndipo mlezi anapoweza kuwa na nafasi ya kuwaongoza vijana wake katika hatua nyingine ya katekesi. Uinjilishaji ni kama kuwanywesha vijana katika imani, na katekesi ni kama kuwazamisha katika imani.
Fungu hili la “Safari ya Kwenda Emau” lina hatua mbalimbali za adhimisho la Misa Takatifu:
- Hatua ya kwanza ni ile ya Ibada ya Kuingia : Hatua hii ni ya kujenga mahusiano, kwa kukaribishana na kila mmoja kujisikia nyumbani.
- Hatua ya pili ni ile ya Liturjia ya Neno la Mungu : Hatua hii ya uinjilishaji huwasaidia watu kutafakari kwamba Neno la Mungu lina maana hasa wakati wa mahangaiko ya maisha yao.
- Hatua ya tatu ni ile ya Liturjia ya Ekaristi: Hatua hii ni ya katekesi ambayo huwasaidia waumini kumtambua Yesu mfufuka katika kuumega mkate.
- Na hatua ya mwisho ni ile ya Ibada ya Kumalizia : Katika sehemu kila mmoja hutumwa kuwa mtume kwa mwenzake.
Hizi kama tunavyoona pia ni hatua za Utume kwa vijana.
Hivyo basi, tunaona kuwa baada ya kujenga uhusiano nao, na kushirikiana nao Neno la Mungu, basi Yesu anawasindikiza hadi mezani. Mlo ni ishara ya ushirikiano wa hali ya juu. Anarudia hatua zile zile alizowahi kufanya katika Mlo wa Mwisho. Ndipo macho yao yalipofumbuliwa.
Liturjia iliyoandaliwa vizuri ni njia ya pekee ya katekesi. Vijana wanayo ari kubwa ya kuonja uwepo wa Mungu, na kuguswa naye. Liturjia inayoadhimishwa kwa moyo wa ibada, kwa mtindo wa kuhamasisha ushirikino, huwa inawasaidia vijana kuwa na mang’amuzi ya Yesu Mfufuka.
Lengo la Utume ni Nafsi ya Yesu Mfufuka
Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao.
Basi, wakaambiana, “Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?” (Lk 24: 31-32)
Yesu amewafikisha katika kilele cha safari yao. Macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua. Kwa vile kazi yake Yesu ilikuwa imefikia tamati, yeye akatoweka kati yao. Yesu anaendelea kuwepo kati yao kwa namna tofauti. Mang’amuzi haya yalikuwa ya kina sana mpaka wanaambiana, “Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu.”
Lengo kuu la utume kwa vijana ni kuwasaidia kumfikia Yesu Mfufuka. Michezo yote, maadhimisho yote, na majadiliano yote ya vikundi vya vijana ni kuwasindikiza katika safari yao ya kumtambua Yesu. Kama vijana wamekwisha kufikia kilele hiki, mlezi anaweza kutoweka. Pengine ni lazima mlezi atoweke, ndipo vijana wanaweza kuendelea na safari yao. Yaani, safari ya kueneza Injili.
Utume kwa Rika
Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu; wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao wamekusanyika wakisema, “Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni.” Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate. (Lk 24: 33-35)
Mtu yeyote aliyeguswa na Habari Njema hawezi kunyamaza. Bikira Maria mara baada ya kupashwa habari na malaika Gabrieli “alifunga safari akaenda kwa haraka” kumlaki binamu yake Elizabeti (Lk 1: 39). Tukio la kusindikizwa na Yesu njiani kwenda Emau, hadi walipomtambua Yeye kuwa Mfufuka, lilikuwa la uzito sana hawakuweza kunyamaza. Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu. Wale waliokuwa wanatoroka kutoka Yerusalemu kwa hofu ya wayahudi, pengine kwa kuchanganyikiwa kwa maneno ya matukio yale ya Ijumaa kuu sasa wanathubutu kurudi Yerusalemu. Wamepata nguvu ya kuendelea na utume wao.
Baada ya kuwafikisha vijana katika mang’amuzi ya Yesu Mfufuka, mlezi anaweza kutoweka, kwa sababu sasa anao mitume wengine ambao wataendeleza utume wake. Huu ndio Utume kwa Rika (Peer-Ministry). Vijana wenye imani dhabiti wana uwezo mkubwa wa kueneza Injili. Vijana wanaposikia Habari Njema kutoka kwa vijana wenzao wanaguswa zaidi.
Hatua hizi za utume kwa vijana si rahisi, pengine huchukua muda mrefu. Utume wa namna hii unaweza kumkatisha tamaa mlezi wa vijana. Mlezi anapoanza kukusanya vijana na kucheza, kwenda piknik, na kuwapa burudani, anaweza kuwa na idadi kubwa ya vijana. Lakini mlezi anapoanza kuinjilisha na kutoa changamoto, vijana watatoweka, na idadi inaweza kupungua. Katika hatua hizi inampasa mlezi kuwa na imani na kuendelea na hatua zinazofuata. Kama mlezi alianza na vijana mia moja na hatimaye amewasaidia vijana kumi au hata watano kumtambua Yesu, basi anaweza kuvuna mavuno mengi tu, kwa sababu sasa watano zaidi watakuwa wanafanya kazi yake.
(Itaendelea…)