UTUME KWA VIJANA 6
Sahaya G. Selvam, SDB
Vyama Mbalimbali na Malezi ya Vijana
Kuwapenda watu, na kupendwa na watu ni mojawapo ya mahitaji ya kila binadamu. Hitaji hili linaamshwa wakati wa ujana. Hali hii hutokana na mabadiliko ya kimaumbile, kihisia na ya kiakili yanayotokea wakati wa ujana. Ndiyo maana vijana huwa wanahangaika sana na suala la kutafuta marafiki na namna ya kukuza mahusiano na watu, hasa uhusiano na watu wa jinsia tofauti.
Malezi ya jumla kwa vijana yanapaswa kuwapa vijana nafasi ya kukomaa kihisia na kijamii. Ukomavu huu unaweza kukamilishwa kwa njia ya vikundi na vyama vya vijana. Hakuna anayeweza kujifunza namna ya kujenga mahusiano yanayofaa isipokuwa kwa njia ya kupata nafasi ya kuwa katika mazingira ya kuzoeana na watu. Kazi ya vyama vya vijana ni kuwatengenezea vijana mazingira haya. Vijana wenyewe wanapenda sana kujiunga na vikundi mbalimbali na kushiriki katika shughuli za vikundi kwa sababu ya hitaji lao la kupenda na kupendwa.
- 1. Anza na Mwisho
Mtu hawezi kuanza safari bila kujua analenga kufikia wapi. Vilevile, mtu hawezi kufanikiwa katika shughuli yoyote bila kuwa na malengo maalumu. Kwa hiyo, chama cha vijana hakina budi kuwa na malengo. Ukweli ni kwamba, lengo la undani la kila chama ni kuwapa vijana nafasi ya kujenga mahusiano na watu, kama tulivyosema hapo awali. Lakini vijana wanaweza kujifunza namna ya kujenga mahusiano na watu hasa pale wanaposhirki katika shughuli mbalimbali zenye malengo maalumu.
Mara nyingi walezi wa vijana wamekuwa wakiunda vyama bila kuwa na mwelekeo mahususi, na wakati mwingine walezi huunda vyama wakiwa na malengo ya muda mfupi tu. Bila ya kuwa na malengo maalumu kikundi kinaweza kuwa kama genge, yaani, mkusanyiko wa watu wasio na utaratibu. Na matokeo ya genge la namna hii ni fujo na uharibifu wa maadili.
Si lazima malengo ya chama yawekwe wazi wanapokutana siku ya kwanza. Suala la kuzingatia hapa ni kuwa, kadiri siku zinavyokwenda basi, inafaa mlezi awasaidie wanachama ili waweze kutambua na kuboresha malengo ya chama chao. Malengo haya yasiwe ya muda mfupi, vilevile yasiwe mapana sana. Kwa msaada wa mwezeshaji fulani, wanachama wasaidiwe kuandika au kuweka wazi tamko la azimio lao. Na azimio hili lililotungwa na wanachama wote liwe linaeleweka kwa kila mmoja. Azimio la namna hii hulinda umoja katika chama. Lakini malengo hasa ya kikundi yatategemeana sana na aina ya kikundi.
- 2. Aina za Vyama
Hadi sasa tumekuwa tukizungumza juu ya umuhimu wa vikundi na hali kadhalika kuhusu umuhimu wa kuwa na malengo katika vikundi. Endapo kama tutakuwa na malengo mbalimbali tunaweza vilevile kuwa na aina mbalimbali za vikundi. Hivi hapa ni baadhi ya aina za vyama ambavyo tunaweza kuwa navyo:
i. Vyama vya Kiutume
Vyama hivi vinaundwa kwa ajili ya kutekeleza utume maalumu katika Kanisa. Kwa mfano, kuna chama cha Bikira Maria, chama cha watumishi wa altare, chama cha Mt. Alois, n.k. Vyama vya namna hii huwa vinaongozwa kwa msimamo wa imani; kwa hiyo, malengo yake huwa ni ya kuwakuza vijana kiimani.
ii. Vyama vya Burudani (Interest Groups)
Hivi ni vyama vinavyoundwa ili kukidhi nia na malengo maalumu ya vijana. Kwa mfano, wanaweza kuwepo vijana wanaopenda kucheza mchezo fulani, kama vile, mpira wa mguu, au hata mpira wa kikapu, vijana wa namna hii wanaweza kusaidiwa kwa kuunda kikundi kinachosimamia utoaji wa mazoezi ya pamoja, na hatimaye malezi yanaweza kutolewa kwa kupitia kikundi hicho.
iii. Vyama vya Rika
Tukilinganisha na tamaduni za mabara mengine katika bara la Afrika, vijana hasa wanapenda kuzoena na wengine wa rika lao. Katika mazingira ya shule au kanisa, njia mojawapo ya kuhakikishia kwamba vijana wanapata malezi bora ni kuwaweka pamoja katika vikundi vya rika. Vyama vingi vya vijana katika parokia zetu ni vya aina hii. Tatizo kubwa la vikundi hivi ni kwamba mara nyingi, kutokana na ukosefu wa ufuatiliaji, wanachama hawapati malezi yanayofaa; na hatimaye vikundi hivi huwa vinafifia vyenyewe. Au basi chama kikiwepo huwa kinaendelea bila lengo maalumu, vijana wanakusanyika kwa sababu ya kufuata mkumbo, na muda mwingi unapotezwa kuzungumzia mambo madogo madogo, kama mchango na mradi, n.k.
iv. Vyama vya Mienendo ya Kitaifa au Kimataifa (Youth Movements)
Vyama vya namna hii huwa mara nyingi ni matawi ya chama fulani ambacho ni cha kitaifa au kimataifa, k.m. YCS, YCW, Scouts, Focolare, CARYM, n.k. Mara nyingi vyama hivi vina katiba zao, na malengo yao pamoja na mfumo wa vikundi huwa vinawekwa wazi. Katika vyama hivi vyote vijana wanaombwa kujiunga kwa hiari yao wenyewe na wala si kwa kulazimishwa. Vyama hivi vinawapa vijana nafasi ya kukutana na vijana wenzao wa mazingira tofauti, na hivi kukuza upeo wao.
Katika taasisi yoyote ya vijana, iwe shule, parokia, au kituo cha vijana, ni muhimu basi kuwepo na vyama vya aina mbalimbali ambavyo vinawashawishi vijana kujiunga na vyama mbalimbali kadiri ya upendeleo wao. Hivyo, tunaweza kuwasilisha malezi kwa vijana kwa kupitia shughuli mbalimbali katika vikundi hivi.
3. Aina za Shughuli Katika Vyama vya Vijana?
Ingawa kila kikundi kitakuwa na shughuli zake kadiri ya malengo yake, ni vyema kuhakikisha kwamba shughuli za kikundi kinaendana na malezi ya jumla ya vijana ambayo tumewahi kuzungumzia katika mojawapo ya makala zilizopita. Kwa maana hiyo basi, shughuli za vikundi ziwe zile zinazomsaidia kijana kukua kiakili, kiroho, kihisia na kimwili.
i. Shughuli za kimwili
Shughuli zinazofanyika katika vikundi zinaweza kuanza na mambo ya burudani, kama michezo, pikiniki, muziki, n.k. Mambo haya huwa yanajenga vikundi, vilevile yanajenga kijana. Na yanatimiza hitaji muhimu la vijana. Shughuli hizi ziwe zinaambatana na shughuli zifuatazo.
ii. Shughuli za kiakili
Binadamu ni mwenye akili pia. Shughuli za vijana hazina budi ziwape vijana nafasi ya kujikuza kiakili. Lengo la kukuza akili za vijana linaweza kutimizwa katika vikundi vyao kwa njia ya shughuli kama semina, hotuba pamoja na majadiliano, mashindano ya maswali na majibu, n.k. Je, hii siyo wajibu wa shule? Ni kweli. Hata hivyo, kama vile shule inawajibika kuwasaidia vijana kujikuza hata kijamii na kiroho, vikundi vya vijana hata vile vilivyopo katika mazingira ya kanisa vinawajibika katika kuwakuza vijana kimwili na kiakili. Hii ndiyo dhamira ya malezi ya jumla.
iii. Shughuli za kihisia na kijamii
Kujiunga na vikundi kwenyewe kunawasaidia vijana kukua kihisia na kijamii, kwa sababu katika vikundi wanapata nafasi ya kukutana na vijana wa rika yao. Tena, kwa njia ya shughuli za pamoja wanajifunza namna ya kuelewana na kuheshimiana. Mambo kama michezo na burudani pia ni nafasi nzuri ya kujifunza stadi za kijamii, kwa sababu, mara nyingi burudani huwa inafanyika pamoja na watu wengine. Licha ya hayo, mambo yale kama majadiliano yanayolenga kushirikishana kwa undani historia ya maisha ya mtu binafsi, pamoja na mazoezi yanayosaidia katika kujitambua na kutambua hali na jamii, yanaweza kukuza vijana kihisia na kijamii.
iv. Shughuli za kiroho
Vikundi vilivyopo katika mazingira ya kanisa vinalenga hasa maendeleo ya vijana kiroho. Vikundi hivi vinawasaidia vijana kufikia mang’amuzi ya Kikristu na hatimaye kuwa mitume wake Yesu katika mazingira yao. Mafanikio ya lengo hili yatapatikana endapo shughuli hizi za kiroho zitafanyika kwa mtindo wa kijana. Mara nyingi hata mambo mazito yanaweza kutolewa kwa njia ya kuwafurahisha vijana. Hivyo, mambo ya kiroho hayatakuwa magumu na ya uzee tu, bali yatakuwa yale yanayoleta furaha ya kweli na tena ya kijana! Sala za pamoja, liturjia iliyoandaliwa vizuri, nafasi za mafungo ya kiroho (ritriti), kusoma na kutafakari Biblia ni baadhi ya shughuli za kiroho ambazo zinaweza kufanyika katika vyama vya vijana.
Kwa namna hii vyama vya vijana vitakuwa mazingira ya kutolea malezi ya jumla kwa vijana. Katika makala itakayofuata tutazungumza kwa undani zaidi mambo mengine yanayotia chachu katika vyama vya vijana.
(Itaendelea…)