UTUME KWA VIJANA 9
Sahaya G. Selvam, SDB
“Tumekuja Kumwabudu”
Siku ya Vijana Duniani na Utume Kwa Vijana
Tarehe 16 hadi 21, mwezi Agosti, mwaka 2005 vijana wapatao millioni moja wanatarajiwa kukutanika huko Koloni nchini Ujerumani. Kongamano hili limekuwa maarufu sana na linajulikana kwa jina la “Siku ya Vijana Duniani” – World Youth Day. Siku ya Vijana Duniani (SVD) huadhimishwa kila mwaka katika majimbo ya Kanisa Katoliki siku ya Jumapili ya Matawi. Lakini mara kwa mara huadhimishwa kimataifa, kwa muda wa wiki moja, kama hii ya mwaka huu huko Koloni. Kwa kawaida, kabla ya wiki ya kongamano lenyewe vijana hukaribishwa katika majimbo mbalimbali ya nchi husika. Wiki kabla ya SVD katika majimbo inawapa vijana wageni nafasi ya kushiriki katika maisha ya vijana wenyeji, na kubadilishana mawazo kuhusu matatizo ya dunia na hali ya Kanisa. Wiki ya “World Youth Day” yenyewe ina vipindi vya Katekesi, nafasi za sala, na hija; wiki ya kongamano hufungwa kwa mkesha pamoja na Baba Mtakatifu. Aidha, washiriki hupata nafasi ya kuadhimisha ujana wao katika sherehe za kiutamaduni zinazofanyika kila siku ya kongamano.
Historia Fupi ya Siku ya Vijana Duniani
Mwaka wa 1985 ulitangazwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Mwaka wa Vijana Kimataifa. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II pia alitangza mwaka huo kuwa Mwaka wa Yubilei katika Kanisa Katoliki. Kuunganisha dhamira hizi mbili Papa aliwaalika vijana wa dunia kukutanika huko Roma kwa ajili ya Siku ya Vijana Duniani mwaka 1984. SVD ilirudiwa tena huko Roma, mwaka 1985. Baba Mtakatifu alihimiza kuwa matunda ya adhimisho hili la kimataifa yashirikishwe katika ngazi ya kanisa mahalia, yaani, katika majimbo na parokia.
Tangu wakati ule SVD huadhimishwa kila mwaka katika ngazi ya jimbo duniani kote siku ya Jumapili ya Matawi. Kila baada ya miaka miwili au mitatu SVD hudhimishwa kimataifa katika mji teule. SVD itakayofanyika huko Koloni mwaka huu itakuwa ya ishirini katika mfululizo wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Siku ya Vijana Duniani – Sherehe za Kimataifa
Mwaka | Mahali | Idadi ya Waliohudhuria |
1984/85 | Roma, Italia | 300,000 (Mara mbili) |
1987 | Buenos Aires, Argentina | 900,000 |
1989 | Santiago de Compastela, Espania | 400,000 |
1991 | Czestochowa, Poland | 1,600,000 |
1993 | Denver, Marekani | 500,000 |
1995 | Manila, Philippines | 4,000,000 |
1997 | Paris, Ufaransa | 1,200,000 |
2000 | Rome, Italia | 2,000,000 |
2002 | Toronto, Canada | 800,000 |
2005 | Koloni, Ujerumani | ? |
Siku ya Vijana Duniani na Malezi ya Vijana
Je, makongamano kama SVD yana faida gani? Je, matamasha ya vijana si nafasi za fujo, tena ni matumizi ya hela bure?
Kadiri ya maoni ya Baba Mtakatifu, maadhimisho ya SVD yana malengo matatu:
SVD ni adhimisho la matumaini : yaani, maadhimisho haya yanatambua nguvu ya vijana duniani, hivyo ni matukio ya kuwatumainia vijana. Vilevile maadhimisho haya yanawatia vijana matumaini. Vijana wanapokutanika kutoka kila upande wa dunia wanadhihirisha matumaini na nguvu wanayochangia kwa kanisa la leo.
SVD ni wito kwa vijana wa dunia kukusanya nguvu zao pamoja. Vijana wana uwezo mkubwa wa kuleta mapinduzi duniani na katika kanisa. Maadhimisho ya SVD yanawapa nafasi ya kutambua nguvu zao, na hivyo kuwa na matumaini kwamba dunia mpya inawezekana kuumbwa.
SVD ni nafasi kwa vijana kukutana na vijana wenzao kutoka mataifa, lugha, mila, na makabila mbalimbali. Maadhimisho haya ya kimataifa yanaonesha ramani halisi ya kanisa la leo. Katika karne hii ya utandawazi adhimisho la SVD linatoa nafasi kwa vijana wa kila nchi na utamaduni kusikika na kuonekana.
Sehemu ya Kongamano la vijana katika Malezi yao
Kwa ujumla, kongamano la vijana linapotayarishwa vizuri linachangia katika kuwaimarisha vijana kiimani na kimaadili. SVD yenyewe ni nafasi nzuri kwa katekesi ya vijana. Kufuatana na mfano wa SVD namna gani tunaweza kufanikisha makongamano ya vijana katika mazingira yetu – yawe “Easter Conference”, au adhimisho la SVD kijimbo, au tamasha lolote la vijana? Nipendekeze mambo machache ya kuzingatia katika kufanikisha kongamano la vijana:
- Dhamira inayofaa ichaguliwe kwa kila kongamano. Inasaidia pia endapo maelezo juu ya dhamira yatasambazwa kwa washiriki wote mapema sana. Vijana waalikwe kukutana katika vikundi vyao kutafakari juu ya dhamira kwa miezi kadhaa kabla ya kongamano.
- Utaratibu wa kuandikisha washiriki kwa kupitia vikundi vyao uanze mapema sana. Uandikishaji usimamishwe wiki kadhaa kabla ya tukio. Hivyo, wahusika wanaweza kuhakikisha idadi ya washiriki mapema sana, vilevile washiriki wenyewe wanapata nafasi ya kuelewa nia ya kongamano.
- Kila mshiriki achangie kiasi fulani katika gharama za kongamano. Vijana wenyewe wanapochangia wanapenda kufaidika na kongamano hilo, hivyo watashiriki kikamilifu zaidi katika tukio.
- Kufanikisha kongamano la vijana tunahitaji kutumia vizuri uwezo wa vijana wenyewe kuwaelekeza vijana wenzao. Kama sehemu ya maandalizi, ni muhimu kuwaalika viongozi na wasaidizi, na kuunda kamati mbalimbali. Ingawa watu wazima wanaweza kusimamia kamati hizi, inafaa kwa vijana wenyewe kuwajibika. Waelewe vizuri malengo na utaratibu wa kongamano, wasaidiane katika maandalizi, na wapewe wajibu wa kuelekeza vijana wenzao wakati wa kongamano.
- Maandalizi ya kongamano, kwa ujumla, yalingane na idadi ya washiriki wa kongamano. Kama kamati ya wanaoandaa kongamano ikiona kwamba nafasi ya kutolea malazi na mahitaji kwa washiriki ni hafifu, ni afadhali kuwa na washiriki wachache. Idadi kubwa ya washiriki itadai maandalizi makali.
- Kila mshiriki apewe kitambulisho na vifaa vingine pamoja na ratiba nzima ya kongamano kabla ya kuanza kongamano. Na wakati wa kongamano yawepo na maelekezo ya kutosha kwa vijana washiriki kuhusu utaratibu wa kongamano.
- Vyakula, vinywaji na malazi yawe ya rahisi kupanga na kuyashugulikia. Washiriki waelewe wanaweza kutazamia aina gani ya vyakula na malazi katika kongamano. Kila mshiriki anapoandikisha akubali kupokea vizuri atakayopewa kama vyakula na malazi.
- Mtindo wa kuchambua dhamira ya kongamano utumie mbinu shirikishi. Kongamano liwe na nafasi ya kutosha kwa vijana kufahamiana wao kwa wao, kusali pamoja na peke yao, kutafakari juu ya dhamira, kushirikisha mawazo kati yao hasa juu ya dhamira, na hatimaye kuwa na maazimio ya kongamano.
- Baada ya kongamano uwepo ufuatiliaji wa vikundi vya washiriki kwa njia ya tathmini, pamoja na utekelezaji wa maazimio ya kongamano.
Tumekuja Kumwabudu (Mt. 2:2)
Kila adhimisho la SVD lina mada yake. Dhamira ya adhimisho la mwaka huu ni, “Tumekuja Kumwabudu”.
Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu, wakauliza, “Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu.” (Mt. 2:1-2)
Dunia hii ya leo inaabudu mambo mengi ya ubatili – mali, mafanikio, mapenzi! Vijana wa siku hizi pia wanavutiwa kuyaabudu mambo yale ya kidunia. Kanisa linaendelea kuwa kama nyota, likionyesha mahali anapopatikana Mfalme Wetu – Yesu Kristu. Vijana wengi hawana muda wa hata kuitazama nyota hiyo. Wengine huwa wanaiona nyota hiyo lakini wanapotea njiani – kwa majumba ya wafalme wa dunia hii. Hivyo wanapotea katika njia panda ya maisha yao, na kukatisha safari ya kuutafuta ukweli na maana halisi ya maisha yao. Katika nafasi hii ya SVD Baba Mtakatifu anawaalika tena vijana wote wa dunia waitazame nyota ile, na kwenda kumwabudu YEYE aliye Muumba wa Dunia, badala ya kuviabudu viumbe vyake.
Baba Mtakatifu Johane Paulo II ametangaza mwaka huu (Mwezi Oktoba 2004 hadi Mwezi Oktoba 2005) kuwa mwaka wa Ekaristi Takatifu. Katika mwaka huu basi, maneno haya – “tumekuja kumwabudu” yanapata pia maana nyingine. Njia ya pekee kumwabudu Yesu ni katika umbo la Ekaristi Takatifu. Basi, wale wataalamu wa nyota “wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia.” (Mt. 2:11) Papa anawaalika vijana wa dunia, kama wale wataalamu wa nyota, waingie makanisa yetu, wamtambue Yesu katika umbo la mkate, wakisaidiwa na Bikira Maria, ili vijana wapige magoti na kumsujudia Yesu Ekaristi.
Wataalamu wa nyota baada ya kumwabudu Yesu, walionywa katika ndoto wasimrudie Herode; “hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine.” (Mt. 2:12) Ni tumaini la kanisa kuwa kwa njia ya tukio kama hili la SVD vijana “watarudi makwao yao kwa njia nyingine”. Yaani, wataonja mageuzi ya maisha ya kiroho, ili waendelee kumwabudu Mungu wa kweli katika maisha yao ya kila siku.
(Itaendelea…)