Maisha ya Kiroho – 1

UTUME KWA VIJANA 10

Sahaya G. Selvam, SDB

 

Vijana, Tunaitwa kuwa Watakatifu!

Maisha ya Kiroho Kwa Vijana – 1

 

Sote Tumeitwa kuwa Watakatifu

 

Mtaguso wa pili wa Vatikano ulitukumbusha kuwa sisi sote tumeitwa kuwa watakatifu:  “Bwana Yesu, aliye Mwalimu na mfano wa kimungu wa kila ukamilifu, aliwahubiria wafuasi wake, wote na kila mmoja wa kila cheo na hali, utakatifu wa maisha, ambao Yeye huwa mtungaji na mtimilizaji wake. ‘Muwe wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu’ (Mt. 5:48).” (Hati ya Mwanga wa Mataifa, na. 40)

 

Kila mmoja katika maisha yake ya kila siku, anatafsiri agizo hili la Yesu kadiri ya nafasi yake na tena kulingana na wito wake – kama mlei, mtawa au padre.   Ingawa kila mmoja anaishi maisha yake kwa namna tofauti, wito wa kuwa mtakatifu ni mmoja.  Katika miaka iliyofuata Mtaguso wa pili wa Vatikano kanisa limeonesha wazi kwamba kuwa utakatifu si jambo la zamani, wala si nafasi pekee kwa wamonaki tu.  Kudhihirisha ukweli huu, kati ya mwaka 1978 na 2005 hayati Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alitangaza watu 469 kuwa Watakatifu na wengine 1314 kuwa Wenyeheri, kati yao wakiwemo walei na hasa vijana.

 

 

Hata Vijana Huitwa Kuwa Watakatifu

Soma hadithi zifuatazo za vijana na kujibu maswali yafuatayo:

  • Nani kati ya vijana wanne wa hapa chini wanaelekea kuwa watakatifu? Na kwa nini?
  • Unaona mambo gani yanayolingana au kufanana katika safari yao ya kuwa watakatifu?

a. Edwin ni kijana mwenye akili na anasoma chuo kikuu.  Alizaliwa katika familia nzuri, ingawa baba yake amekuwa mlevi.  Edwin anaamini kuwa Mungu anampenda, na yeye anatakiwa kuitikia upendo huo kwa njia ya kutumia vizuri vipaji alivyo navyo.  Huyu Edwin ni kijana mwenye furaha daima, aliyeridhika na maisha; ana marafiki wengi hata wasichana. Mara kwa mara anapenda kuwasaidia dada zake jikoni.  Kwa ujumla, Edwin  anapenda kuishi maisha yake vizuri sana, anawapenda watu, na ni mtu mwaminifu.

 

b. Anne ni wa kabila la wachungaji.  Amebahatika kuingia shule ya sekondari.  Shuleni anaongoza kwaya, na mshiriki mzuri katika kikundi cha vijana.  Ni mchangamfu, lakini katika mambo mengine ni mwenye msimamo mkali; mara nyingine wenzake huwa wanamwita “mshamba”. Wanadhani kwamba yeye anataka kuwa mtawa, lakini mweyewe Anne anafikiria kuwa utawa si wito wake. Anataka kuwa mwaminifu kwa Mungu na kuwa mwenye furaha, basi.

 

c. John amelelewa na mama yake; hajui baba yake.  Baada ya kumaliza kidato cha nne, amebahatika kupata kazi ambayo inampa matumaini makubwa.  John ni mwaminifu katika mahali pa kazi. Anawajibika sana katika kumtunza mama yake, ambaye sasa hawezi kufanya kazi.  Katika muda wake wa ziada John anajishughulisha na utume kwa vijana wenzake; ana mafanikio makubwa katika utume huu.  Kila jioni anawafundisha  pia watoto wa majirani zake.  Kila siku huwa anaenda kanisani; wakati mwingine anapenda sala ya binafsi; anapata mwongozo wa kiroho kwa padre mmoja.  Anavutiwa na wasichana lakini anaamini kwamba atavumilia hadi ndoa kujiingiza katika mapenzi.  Hali ya familia yake, yaani swala la baba yake, linamsumbua, lakini kwa msaada wa padri anaishughulikia kisaikolojia.

 

d. Faith ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza. Si mrembo sana. Anajitahidi katika masomo yake.  Anaamini kwamba Mungu anamwita kuwa mtawa, lakini baba yake amemwambia kufikiria wito wake baada ya kidato cha nne. Faith anashiriki vizuri katika liturjia, na kusali.  Ni mwepesi wa kuzoena na watu wote.  Hasiti kutoa maoni yake bila hofu. Ni mkamilifu katika kutimiza wajibu wake wa kila siku.

 

Tunaweza kusema kwamba wote wanne wanaishi maisha ya utakatifu, kila mmoja kadiri ya nafasi yake.  Hadithi hizi za vijana hawa wanne hazikubuniwa, bali hawa ni vijana wanaoishi katika nchi za Afrika Mashariki.   Mimi binafsi ninawafahamu hawa, na ninawafahamu vijana wengine wengi tu, ambao wanajitahidi kuishi maisha ya utakatifu.

 

Katika kuishi maisha ya kiroho kwa vijana na kuelekea utakatifu tunaweza kuzingatia mambo yafuatayo:

 

1. Inawezekana kwa vijana kuwa watakatifu, tena ni rahisi sana.

 

Vijana wengi mara nyingine huwa wanaamini kwamba kuwa watakatifu ni kujinyima furaha na uchangamfu wa ujana, kwa hiyo wanapenda kuahirisha hatua za kuishi maisha ya utakatifu.  Utakatifu ni kuishi maisha kwa ukamilifu na tena kuishi kwa furaha.  Kwa hiyo utakatifu si hali ya kufikiria katika uzee. Utakatifu ni safari ambayo inatakiwa kuanzishwa mapema katika ujana.  Katika orodha ya watakatifu wa kanisa katoliki wako wengi tu ambao kanisa limekubali kuwa walijikamilisha kiroho wakiwa wadogo, kama, Alois, Teresa wa Mtoto Yesu, Dominiko Savio, Maria Goreti na Kizito.  Hawa ni mifano tu ya waliotangazwa rasmi kuwa watakatifu.  Tunajua kwamba wako wengi hata katika mazingira yetu ambao wanaishi maisha ya utakatifu. Kama hawa wanaweza kuwa watakatifu, hata sisi tunaweza.

 

Ndiyo maana,  hayati Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, aliwahamasisha vijana wa dunia nzima kufuata njia ya utakatifu, “Vijana wa kila bara, msisite kuwa watakatifu wa millenia mpya!  Muwe wapenda wa kutafakari na kusali; muwe wadhabiti katika imani, na wakarimu katika kujitolea kwa ajili ya ndugu wenzenu, na muwe washiriki wachangamfu wa kanisa, na katika kujenga amani duniani.”

 

2. Vijana wanaitwa kuishi utakatifu kulingana na hali yao ya ujana.

 

Kama nilivyosema hapo awali kuishi utakatifu si kujinyima furaha na uchangamfu wa ujana bali ni kuishi maisha kwa furaha ya kweli. Mtaguso wa pili wa Vatikano unatukumbushia, “Katika namna kadha za kuishi na za kutekeleza shughuli mbalimbali, utakatifu ulio mmoja hutafutwa na wote ambao huimarishwa na Roho Mtakatifu…

“Wakristo wote basi, katika hali, shughuli, na mazingira ya maisha yao, na kwa njia ya hayo yote, watazidisha kila siku utakatifu wao….” (Mwanga wa Mataifa, na. 41)

 

Kama kila mmoja anaitwa kuishi maisha ya utakatifu kadiri ya hali yake, basi, vijana wanaitwa kuishi utakatifu kadiri ya ujana wao. Wanatakiwa kutumia nguvu zao za ujana katika maisha ya kiroho.

 

3. Kuwa watakatifu ni kazi ya kujikamilisha

 

Kwa kawaida vijana wana nguvu za ajabu ya kimwili; wanatafuta watu wanaoweza kuwapenda na kupendwa nao; vijana huwa wanatafuta uhuru wa kutumia uwezo wa kiakili; na wanatamani njia ya pekee kumgusa Mungu na kuguswa naye.  Kutokana na hali hii basi wanajaribujaribu mambo mengi, wakitumia vipawa vyao vya kimwili, kimoyo, kiakili na kiroho.  Maisha ya utakatifu ni kweli kujikuza na kujikamilisha katika vipengele hivi vya ubinadamu.

 

Mwinjili Luka anapoeleza ujana wake Yesu anatoa muhtasari mzuri wa hali ya kujikamilisha: “Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.” (Lk. 2:52)  Luka anamaanisha kuwa Yesu aliendelea kukua kiakili (katika hekima), kimwili (katika mwili), kiroho (akazidi kupendwa na Mungu) na kimoyo (kupendwa na watu).  Ujana wake Yesu ulikuwa wa kiutakatifu kwa sababu alikuwa anajikamilisha.

 

Yesu, katika utume wake wa kuhubiri alisisitiza, “Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” (Mt 5:48)  Kwa hiyo, maana ya kuwa mtakatifu ni kujikamilisha.

 

4. Vipengele vya maisha ya kiroho kwa vijana

 

Kutokana na maelezo yetu ya hapo juu, basi tunaweza kuorodhesha vipengele vichache vinavyoendana na maisha ya utakatifu kwa vijana wakatoliki:

i. Adhimisha maisha kwa furaha

ii. Timiza wajibu wako wa kila siku

iii. Pokea msalaba wa maisha yako

iv. Uwe umeunganika na Mungu katika sala

v. Utambue wito wa maisha

vi. Ujihusishe na maisha ya kijamii na kisiasa

vii. Uwe sehemu ya kanisa

 

Katika makala inayofuata tutaeleza kwa undani zaidi vipengele hivi vinne.

 

(Itaendelea…)