Vyama vya Vijana -2

UTUME KWA VIJANA 7

Sahaya G. Selvam, SDB

Mambo Yatiayo Chachu katika Vyama vya Vijana

 

Katika makala iliyopita nilieleza kuhusu umuhimu wa vyama katika malezi ya vijana, niliorodhesha pia aina za vyama pamoja aina mbalimbali za shughuli zinazoweza kufanyika katika vikundi vya vijana.  Katika makala hii ningependa kutaja na kueleza vipengele vichache vinavyosaidia kufanikisha vyama vya vijana.

 

 

1. Mfumo na Uongozi

 

Endapo chama cha vijana kitafanikiwa kutolea malezi ya jumla kwa vijana ni lazima kiwe mfumo mzuri, pamoja na uongozi bora. Ingawa mfumo wa chama unaweza kuwa tofauti kadiri ya malengo yake, hapa tunaweza kutaja mfumo wa jumla ambao unafaa kwa chama chochote kile.  Kila chama kina wanachama wake, na viongozi wake ambao wanachaguliwa au kuteuliwa na wanachama. Uongozi unaweza kuundwa na watu kama watatu au watano kadiri ya mahitaji ya chama. Kuwa na watu wengi katika uongozi hakusaidii sana.   Aidha, kila chama cha vijana lazima kiwe na mlezi, walau mmoja,  ambaye ni mtu mzima, wala si mwanachama. Tunaweza kufanananisha mlezi wa kikundi na kocha wa timu ya mpira ambaye hachezi mwenyewe, ila anatoa mwongozo, kadiri ya malengo yaliyowekwa na wanachama.

 
Katika ngazi ya taasisi au parokia vyama vyote vya vijana vilivyopo vinaweza kuwekwa pamoja (organized)  kadiri ya mfumo ufuatao.

 

 

Yaani, ya kwanza, badala ya kuwa na chama kimoja cha vijana ni afadhali kuwa na vyama vingi.  Si bora kuwa na vijana 20 kwa kila chama, na vijana 80 katika vyama vinne, kuliko kuwa na vijana 40 pamoja katika chama kimoja? Ya pili, walezi wapewe mwongozo kutoka kwa kiongozi wa taasisi au paroko, ili kuwepo na utaratibu ulio sawa katika vyama vyote, ingawa kila chama kitakuwa na malengo yake maalumu.  Ya tatu, viongozi wa vyama vyote waunde Halmashauri ya Vijana Kiparokia au kitaasisi.  Na hatimaye, viongozi wa Halmashauri ya Vijana wapate nafasi ya kuwa wajumbe katika ngazi inayofuata kama Halmashauri ya Kiuchungaji Kiparokia.

 

 

2. Mali na Malezi

 

Michango na mfuko wa fedha mara nyingi ni sababu ya kuvunjika na kusambaratika kwa vyama vya vijana. Katika hali ya namna hii basi, ni afadhali kwa chama chochote, ikiwezekana kudumu bila mchango au mfuko. Lakini kama kweli mfuko wa fedha utahitajika, ningeshauri basi mambo yafuatayo yazingatiwe:

  • Mchango ufanyike kwa lengo maalumu wala si kwa ajili ya kuwa na mfuko tu.
  • Hesabu za mapato na matumizi ziwekwe kikamilifu na kutangazwa wazi mara kwa mara.
  • Utaratibu wa matumizi ya fedha uwekwe wazi na kwa idhini ya mlezi na uongozi. Fedha hiyo, ni vyema, itumike hasa kwa shughuli maalumu kama zile za kukuza na kulea vijana.  Shughuli hizo basi ziwe ni kama kushiriki warsha au semina.  Na siyo kwa ajili ya sherehe tu.
  • Lakini, katika matumizi ya fedha kwa ajili ya wanachama binafsi, kama vile kutoa rambirambi au mchango wakati mwanachama mwenzao amefiwa au ni mgonjwa, wanachama wote washiriki pamoja katika kuufikia muafaka.

 

Ingawa mali au fedha ni muhimu, isipoangaliwa kwa makini, yaweza vilevile kuleta taabu nyingi katika vyama. Mara nyingi fedha zinaweza kuwa kizuizi kwa wanachama kutokutimiza malengo ya chama, na hivyo kuwa kikwazo katika malezi ya vijana.

 

 

3. Mawasiliano na Majadiliano

 

Popote pale watu walikokusanyika ni lazima pawepo na mawasiliano. Kwa hiyo, mawasiliano ni sehemu muhimu katika kufanikisha kikundi. Mawasiliano dhabiti yanaunganisha wanachama, na ukosefu wake unaweza kuwakatishia wanachama tamaa. Mawasiliano katika kikundi  yanaanza na kila mwanachama kuelewa malengo ya kikundi, na kujua sehemu yake katika utekelezaji wa mipango ya kikundi.

 

Mawasiliano kati ya wanachama yanaweza kufanyika kwa njia mbalimbali, kama vile:

  • Matangazo ya mdomo kanisani, redioni, n.k.,
  • Ubao wa kielelezo kwa maandishi,
  • Kwa njia ya barua kwa wanachama ingawa hii ni ya gharama, au hata kwa njia ya barua pepe hasa katika mazingira ya mjini,
  • Na hasa kwa njia ya mkutano wa pamoja.

 

Mikutano ni njia ya kuhakikisha mawasiliano ya ana kwa ana na pia hutoa fursa ya mshindo-nyuma (feedback). Aidha, mikutano na majadiliano hufikia maamuzi pamoja na kwa haraka. Lakini ili kufanikisha mkutano wowote mambo yafuatayo ni ya muhimu:

  • Kuhakikisha kwamba taarifa ya muda na mahali pa mkutano imewafikia wanachama wote.
  • Kuwahi kuanzisha mkutano kadiri ya muda.  Kwanza, viongozi wenyewe kuwahi, na kuwasisitizia wanachama kuwahi.
  • Mkao wa duara unasaidia ushirikiano zaidi kuliko ule wa darasani.
  • Uongozi uwawezeshe wanachama kuchangia maoni yao. Si viongozi peke yao waongee muda wote.
  • Mwenyekiti awe mwenye haki kuwapa wote nafasi ya kutosha, kulinda muda na kufunga mkutano wakati wake. Pengine, majadiliano yakizidi inafaa kwa mwenyekiti kutoa kauli yake ya mwisho.
  • Kuufikia uamuzi wa haraka kwa kunyosha mikono si njia nzuri ya kuamua katika mambo yote na wakati wote.

 

 

4. Mengineyo

 

Kufunga makala hii basi, ningependa kuorodhesha mambo mengine yanayohitajika katika utoaji wa malezi bora kwa vijana, kwa kutumia vyama vyao:

 

i. Kujiunga na Kumwachisha mtu uanachama :

Kila chama kinahitaji kigezo thabiti kuhusu kujiunga na kumwachisha mtu uanachama. Chama kinahitaji mipaka yake.  Isiwe kwamba kijana anakuja kwenye mkutano na anakuwa mara moja mwanachama.  Mwanachama atatakiwa kuwa na hadhi fulani kama vile, umri na msimamo wake. Na ni vyema akapokelewe tu baada ya yeye kuelewa malengo ya chama. Vilevile, ni afadhali kukawepo na ada ya kiingilio walau kiasi kidogo, kwani hii itasaidia katika kuhakikisha nia yake ya kujiunga kikundi, pamoja na hayo ni vizuri kitambulisho kikatolewa kwa kila mwanachama.

Mara nyingi, vyama vingi vya vijana vimekuwa vinakosa kigezo cha kuhitimisha uanachama.  Kwani, mtu hawezi kuwa kijana maisha yake yote, kwa hiyo ni vyema kwa chama chochote cha vijana kuwa na  kigezo cha umri kama miaka thelathini, au kigezo cha kuoa na kuolewa.

 

ii. Noa Shoka

Kufanikisha malengo ya chama, inawapasa wanachama kupata nafasi ya kutathmini mafanikio na matatizo ya shughuli zao.  Wakisha kufanya tathmini wanaweza kujikumbushia malengo na maazimio ya chama.  Vijana daima wanapenda mambo mapya.  Kwa hiyo, malengo ya chama yanahitaji kutafsiriwa kwa ubunifu, kuweka vipaumbele.  Wanachama wanahitaji pia nafasi ya kuburudika, pamoja na nafasi ya kujikuza kiakili kwa njia ya semina na majadiliano ya kina, na kujikuza kiroho kwa njia ya sala na ukimya.

 

(Itaendelea…)