Malezi Jumla

UTUME KWA VIJANA 3

Sahaya G. Selvam, SDB

Malezi jumla kwa Vijana

 

Naye Yesu Akakua…

 

Mtoto Yesu alipoanza kuingia katika ujana wake, akiwa na umri wa miaka kumi na miwili, alianza kutafuta maana ya maisha yake.  Alitaka uhuru zaidi kutimiza malengo ya maisha yake.  Ndiyo maana alikuwa amepotea hekaluni. Alianza kutambua kwamba ilikuwa inampasa kuwa katika nyumba ya Baba yake!  Lakini mwinjili Luka anatuambia kwamba baada ya wazazi wake kumwona,

“Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii…. Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima, na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.” (Lk 2:51-52)

Nafsi ya kila binadamu ina vipengele vinne.  Hivi ni Mwili, Akili, Hisia (Moyo) na Roho. Vipengele hivi vinaendana na mahitaji manne makuu ya binadamu.  Sisi binadamu tunataka kuishi; tunatafuta usalama na raha ya kimwili.  Ya pili, tunataka kujifunza mambo mapya, yaani kukuza akili zetu.  Ya tatu, daima binadamu hutafuta uhusiano na watu; tunataka kuwapenda watu na kupendwa na watu; ndiyo haya mahitaji ya kimoyo. Na ya nne, tunatafuta mang’amuzi ya kimungu. Tunajua kwamba amani na furaha ya kweli tunazotafuta zinapatikana kwa Mungu peke yake.  Ndiyo maana Mt. Augustino baada ya kufanya juu chini kutafuta raha za kidunia, alikubali kukiri, “Mioyo yetu imetengenezwa kwa ajili yako, ee Bwana; na haitatulia mpaka itulie nafsini mwako!”

Ujana ni kipindi cha ukuaji wa pekee.  Ujana ni wakati wa kutafuta namna ya kutimiza mahitaji yetu makuu.  Safari yetu ya kujikamilisha ni kutimiza mahitaji haya, na kujikuza katika vipengele vinne vya mwili, akili, moyo na roho.  Mwinjili Luka anaposema, “Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima, na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu”, anamaanisha kuwa Yesu alikuwa anapewa malezi ya jumla, yaani alikuwa anakua kiakili, kimwili, kiroho na kimoyo au kijamii.

 

Vijana Huhitaji Malezi ya Jumla

 

Utume kwa vijana lazima umjali mtu mzima, katika vipengele vyote.  Malezi ya jumla kwa vijana (Holistic Youth Ministry) ni kuwapa nafasi ya kujikuza kimwili, kiakili, kijamii, na kiroho. Kwa mantiki hii basi, kila kituo cha vijana kinatakiwa kuwa na nafasi ya kukuza vipengele hivi vinne vya binadamu.  Kila kikundi cha vijana kufanikisha malezi ya jumla, kiwe na shughuli zinazoendana na mahitaji ya vijana kujikuza.

Kwa hiyo, kituo kizuri cha vijana kinatakiwa kuwa na nafasi ya vipengele vifuatvyo. Tuzingatie kuwa vifuatavyo hapa chini havimaanishi sehemu ya majengo bali ni nafasi mbalimbali za kukuza mtu mzima.  Pengine nafasi hizi zitaonekana katika ratiba na mazingira ya kituo.

  • Uwanja wa mchezo unaowapa vijana nafasi ya kujiburudisha, na kutunza miili yao. Aidha, uwanja wa mchezo unawapa vijana namna ya kujenga mahusiano.  Kwa hiyo, kituo cha vijana kinatoa nafasi za burudani, kama vile, mchezo, muziki, pikniki, video, n.k.
  • Darasa ambalo linawafundisha vijana maarifa mbalimbali, hivyo hukuza akili zao.  Kikundi cha vijana kinawapa vijana mafundisho, na nafasi nyinginezo kama kusoma vitabu kwenye maktaba, kushiriki katika semina na warsha, kwenda kwenye safari za kielimu, n.k.
  • Kanisa ambalo linawasaidia vijana kuunganika na Mungu. Sala, liturjia zilizoandaliwa vizuri na zinazochochea ushirikiano, majadiliano ya Biblia, retriti (mafungo ya kirohi), nafasi za kutenda matendo ya huruma, n.k. zinaweza kuwapa vijana fursa ya kujikuza kiroho.
  • Nyumbani ambapo vijana wanajisikia kuwa wanakaribishwa.  Wanajisikia kuwa wanapendwa na watu, na wanayo nafasi kujifunza namna ya kuzoena na vijana wenzao. Nyumbani hujengwa na watu.  Kituo au kikundi cha vijana kinaweza kuwa nyumbani kama mlezi wa vijana anaweza kuwa karibu na vijana, kama rafiki, ndugu na mzazi.  Usikivu wa watu wazima, na uwezo wa kutoa nasaha unageuza kituo cha vijana kuwa nyumbani.

Labda mlezi wa vijana atakuwa na wasiwasi: namna gani kikundi cha vijana parokiani kinaweza kuwa na nafasi ya kutoa elimu?  Elimu hutolewa shuleni!  Ni kweli kwamba kipaumbele cha kikundi cha vijana katika mazingira ya parokiani ni kuwasaidia vijana kukua kiroho. Hata hivyo, kila kikundi kina wajibu wa kuwasaidia vijana kukuza nafsi zao katika vipengele vyote, yaani, mwili, akili, roho na moyo.

 

Elimu ya Jumla (Integral Education)

 

Vilevile, hata shule zile zinazowajibika na ukuaji wa kiakili mahsusi, hutakiwa kujali vipengele vingine vya mahitaji ya wanafunzi.  Hati maalumu iliyotolewa na UNESCO (Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa) mwaka 1996, kuhusu vipaumbele vya elimu katika karne ya ishirini na moja, (“Learning: The Treasure Within”, Report to UNESCO of the International Commission on Education for the 21st Century, 1996.) inataja nguzo nne za elimu ya jumla:

1. Kujifunza kujua (Learning to know)

2. Kujifunza kutenda (Learning to do)

3. Kujifunza kuishi pamoja na watu (Learning to live together), na

4. Kujifunza kuwa (Learning to be)

 

Nguzo hizi za elimu zinaweza kutuelewesha zaidi kuhusu malezi ya jumla ya vijana.

 

1. Kujifunza namna ya kujua:

Wajibu wa shule ni kukuza akili za wanafunzi kwa kuwapa maarifa.  Lakini elimu si sawa na maarifa.  Elimu ni ukuzaji.  Ndiyo maana hati ya UNESCO inasema kwamba shule inatakiwa kuwafundisha vijana mbinu za kujifunza, kuliko kuwapa taarifa kadhaa ambazo vijana hutakiwa kumrudishia mwalimu wakati wa mitihani.  Bali elimu halisi hujenga hamu ya kujifunza daima, hata nje ya shule. Zaidi ya taarifa kadhaa, shule inatakiwa kuwafundisha vijana namna ya kuendelea na elimu hadi uzee (life-long education).  Ndiyo, elimu ya shule ni maandalizi kwa ajili ya elimu ya maisha.  Na elimu haina mwisho.

 

2. Kujifunza kutenda

Ujuzi peke yake hautoshi kuwakuza vijana.  Wanahitaji utendaji. Elimu inaendana na ufundi stadi ambao huwawezesha vijana kufanya kazi fulani. Zaidi ya kuwaandaa vijana kwa ajili ya kufanya kazi,  elimu huwaandaa vijana kukutana katika maisha yao ya kijamii, hali tofauti na ya shule.   Kwa hiyo wanahitaji stadi za maisha, kama vile, kujitambua, kujithamini, namna ya kujenga uhusiano na watu, mbinu za kuwasiliana na watu, namna ya kukabili hasira na mshinikizo, jinsi ya kutatua matatizo ya maisha, n.k.  Hivyo, elimu inawaandaa vijana kwa ajili ya maisha.

 

3. Kujifunza kuishi pamoja na watu

Nyakati hizi za utandawazi tunazidi kuishi na watu wa makabila, lugha, mataifa, na desturi na mila mbalimbali.  Ni wajibu wa elimu ya shule kuwawezesha vijana kuishi na watu mbalimbali.  Mtu mwenye elimu ni yule anayeweza kuelewana na watu tofauti na asili yao.  Zaidi na zaidi vijana wanahitaji kupewa nafasi ya kuelewa historia, desturi na mawazo ya watu wa makabila na mataifa mbalimbali.  Vijana wanahitaji kuelewa kwamba njia ya kutatua matatizo kati ya watu ni kwa njia ya mawasiliano na majadiliano.  Vita na mapigano hayana maana katika karne hii ya ishirini na moja.

 

4. Kujifunza kuwa

Mafanikio ya kweli ya mtu hayategemei na ujuzi alio nao wala stadi alizo nazo, bali yanategemea na hali ya nafsi yake mwenyewe.  Elimu inatakiwa kujenga nafsi ya mtu.  Vijana wanahitaji kuelimishwa namna ya kuwajibika katika maisha yao; namna ya kuwa na msimamo dhabiti ya kimaadili; namna ya kutimiza ahadi za maisha yao; na namna ya kuwa raia wema na wakristu wazuri.

 

Kuinjilisha kwa njia ya Kuelimisha

 

Ndugu msomaji, labda unashangaa kwa nini katika mfulilizo wa makala kuhusu Utume Kwa Vijana, na katika makala hii ya Malezi ya Vijana, tumeanza kuzungumza kuhusu elimu.  Katika Chuo chetu cha Mafunzo ya Malezi ya Vijana hapa Nairobi (Institute of Youth Ministry – Tangaza College, CUEA) wanafunzi wanaanza kutambua kwamba mafunzo ya malezi ya vijana yanahusu elimu ya jumla.  Mara nyingi hapa chuoni tunawakumbushia wanafunzi wetu kuwa vyuo vingine vya ualimu huandaa walimu, na sisi tunaandaa wataalamu wa elimu, yaani walezi wa vijana. Kweli, hatuwezi kutenganisha elimu kutoka malezi ya vijana.

Tangu karne ya kumi na tisa fikra za kanisa ni kwamba tunaweza kuwainjilisha vijana kwa njia ya kuwaelimisha, na kuwaelimisha kwa njia ya kuwainjilisha.  Maana yake ni kwamba vijana wanaweza kusaidiwa kuwa wakristu wazuri kwa njia ya kuwapa elimu-dunia na maarifa. Vilevile vijana wanaweza kukua na kuwa watu wenye elimu kwa njia ya emilu-dini na kukuza imani yao. Na elimu halisi hukuza mtu mzima katika vipengele vyote.  Aidha, mazingira ya shule na mfumo wa elimu una sehemu kubwa katika kukuza vijana.

Yesu anasema, “Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Mt. 5:48).  Katika safari yao ya kujikamilisha vijana wanahitaji kusaidiwa namna ya kuunganisha vipengele vyote vya nafsi yao. Haya ndiyo malezi ya jumla kwa vijana.