UTUME KWA VIJANA – 17
Sahaya G. Selvam, SDB
Katekisimu kwa ajili ya Vijana – 2
Utangulizi:
Katika makala iliyopita tulieleza malengo ya “Katekisimu hii kwa ajili ya Vijana” na tulitoa maswali 11 pamoja na majibu yake. Katika makala hii tunaendelea na mfulilizo huo.
12. Kwa nini niungame kwa padre?
Ninapotenda dhambi ninajitenga na Mungu na kanisa (yaani Jumuiya/jamii). Padre kama mwakilishi wa Mungu na kanisa ananipatanisha na Mungu na kanisa. Pili, Mungu asiyeonekana ananijulisha kuwa amenisamehe kwa njia ya vitendo na maneno katika nafsi ya padre anayeonekana.
13. Katika sakramenti ya maungamo nieleze dhambi namna gani?
Ili nipate uponyaji kwa dhambi zangu, niwe nataja tendo nililofanya pamoja na mazingira na lengo lililokuwa nalo nilipotenda dhambi, kama nikiona linaweza kuathiri uzito wa dhambi.
Kwa kweli nikiwa nataja dhambi za jumla (k.m. nilivunja amri ya sita), hivi sitaonja uponyaji mwenyewe. Ninapoeleza wazi dhambi zangu ninaonyesha pia moyo wa majuto pamoja na nia ya kujirekebisha, kwa neema ya Mungu.
14. Mbona sisi Wakatoliki tunawabatiza watoto wachanga kabla hawajatambua maana ya sakramenti wala bila kukiri imani yao?
Ubatizo wa watoto wachanga ni kama hatua ya kwanza tu ya sakramenti za kumwingiza (Sacraments of Initiation) katika Imani. Mchakato huu hukamilishwa katika sakramenti za Ekaristi na Kiipaimara ambazo atazipokea akiwa na ufahamu.
15. Nani ni mhudumu wa sakramenti ya ndoa?
Ni wanandoa wenyewe. Kila mmoja anampa mwenzake sakramenti ya ndoa.
Padre katika adhimisho la sakramenti ya ndoa hatoi sakramenti (kama anavyotoa Kitubio au Ekaristi), ila yeye anasimama kwa niaba ya kanisa kulibariki na kuliidhinisha agano linalowekwa na wanandoa. Wanandoa ndio wahudumu wa sakramenti ya ndoa.
16. Taja malengo makuu matatu ya ndoa za kikristu?
Ndoa ya kikristu ina nguzo tatu, ambazo ni upendo wa kindoa kati ya wanandoa, haki ya kujifurahisha kijinsia na kuzaa watoto kadiri ya uwezo wao na mapenzi ya Mungu.
Katika ndoa ya kikristu upendo kati ya wanandoa ni muhimu sana. Aina hii ya upendo ni tofauti na upendo kati ya marafiki au ndugu. Upendo huu unadhihirishwa katika tendo la ndoa. Upendo huu unaweza kudumu bila watoto. Lakini wanandoa wasiwe wachoyo wa kushirikisha uhai wao na kizazi kingine.
17. Je, ndoa inaweza kuwa ndoa bila watoto?
Ingawa ni kosa endapo wanandoa wataamua kutokana na ubinafsi wao wasiwe na watoto, kama hawana watoto kutokana na sababu nyingine ndoa hiyo bado ni ya kikristu.
18. Je, kanisa linaruhusu uzazi wa mpango?
Kanisa linapendekeza uzazi wa kuwajibika (responsible parenthood). Kwa maana kwamba wazazi wakristu wazae tu watoto ambao wenyewe wanaweza kuwatunza na kuwaelimisha.
Ila kanisa linapinga mbinu za bandia zinazotumika kuzuia mimba kwa sababu zinahatarisha uhai na utu wa binadamu. Mbinu nyingine zinatoa mimba siyo kuzuia, hivyo zinauhatarisha uhai. Mbinu nyingine zinaingiza ubinafsi katika tendo la ndoa, hivyo zinauhatarisha utu. Papa Paulo VI, katika hati ya Humanae Vitae (na.10), anasema, Uzazi wa Kuwajibika ni kutambua vipengele vya kibiologia vya kuzaa, kutambua na kujitawala katika mvuto wa kijinsia, kupokea watoto kama zawadi kutoka kwa Mungu, vilevile baada ya kutafakari kuwa na idadi ile tu ya watoto ambayo wazazi wanaweza kuwatunza vizuri; na katika mambo haya yote kufuata dhamiri iliyo hai, kuheshimu mpango wa Mungu na kuzingatia manufaa ya jamii na kanisa.
19. Je, Mungu aliviumba vitu vyote vikiwa vilivyo kama Biblia inavyosema au viligeuka kuwa hivyo kama sayansi inavyosema?
Mungu aliviumba vitu vikiwa na uwezo wa kuendelea kujigeuza wenyewe katika maumbo yao.
Tayari mwaka 1950 hati ya Baba Mtakatifu Pio XII imewahi kukubaliana na maoni haya: Kanisa linaruhusu utafiti kufanyika kuhusu nadharia ya mageuzi (evolution) mintarafu asili ya mwili wa binadamu, wakati kanisa linaendelea kusisitiza kuwa asili ya roho ya binadamu ni Mungu mwenyewe. Na.36.
20. Nani ameniumba?
Ni Mungu kwa kushirikiana na wazazi wangu.
Mungu alimwumba mwanadamu wa kwanza (Adamu) kwa namna ya pekee, akaweka kipengele cha roho ndani yake (Mwa 1: 26-27; Zab. 8:5); vilevile katika kuzaliwa kwangu Yeye ndiye alinitunga kwa namna ya ajabu ndani ya tumbo la mama yangu (Zab.139:16)!
21. Kwa nini Mungu ameniumba?
Ili nifurahie maisha ya kibinadamu, nichangie katika furaha ya wengine na hivyo kumtukuza Mungu na hatimaye kufurahi daima pamoja naye.
Mtakatifu Ireneo aliwahi kusema, “Binadamu aliye hai ni utukufu wa Mungu.” Tena katika mfano wa mwana mpotevu (Lk 15:11-32) tunaona kuwa yule kaka aliyekuwa anamtumikia baba na kutii amri zake, hatimaye alikataa kuingia katika adhimisho la sherehe.
Furaha ya kweli katika maisha ya hapa duniani ni utangulizi wa furaha ya milele. Na furaha ya kweli ni tofauti na hali ya starehe au kujiburudisha au kujifurahisha. Furaha ya kweli ni hali ya ndani na inadumu hata katika taabu. Kujifurahisha kunategemea mambo ya nje na kunayeyuka, pengine kunatuachia katika hali ya hatia na majuto.
22. Namba gani ninaweza kuwa na furaha ya kweli?
Kwa njia ya kuutambua mpango wa Mungu katika maisha yangu ya kila siku; na kuutimiza mpango huo.
Tunatakiwa kutambua na kutimiza mpango wa Mungu kadiri ya uwezo wetu. Mpango wa Mungu kwangu ni ili niwe na furaha ya kweli. Mungu anaelewa kuliko hata mimi mambo gani yataniletea furaha ya kweli, kwa hiyo ninajitahidi kuelewa kadiri ya uwezo wangu mapenzi ya Mungu kwangu ili niwe na amani na furaha ya kweli moyoni mwangu.
23. Je, nisipotimiza mpango wa Mungu katika maisha yangu nitaenda motoni?
La hasha! Bali huwezi kuridhika na maisha. Tena utaacha pengo katika historia ya dunia ambalo ulitakiwa kujaza.
Mungu ametuumba kila mmoja wetu kwa lengo maalumu, tusipolitimiza tunaacha pengo kubwa katika historia ya ubinadamu. Kuishi maisha ya furaha ya kweli hapa duniani na katika maisha ya baadaye itategemea na uamuzi wangu, kutokana na ufahamu na utashi wangu (angalia maswali hapo juu 9 na 19). Mungu anaheshimu utashi wangu.
24. Je, Mungu angalijua kwamba Adamu ataanguka si afadhali angalizuia kabla?
Kwanza, Mungu hana wakati uliopita wala wakati ujao. Pili, uwezo wa Mungu unaisha pale utashi wa binadamu unapoanza. Mungu ameniumba na utashi wangu ambao naweza kuutumia hata kumkana Mungu. Ndivyo ilivyokuwa katika dhambi ya kwanza.
25. Je, Mungu anaweza kunipeleka motoni?
Itategemea na uamuzi wako kwa kutumia akili na utashi wako.
Yaani, tulivyosema hapo juu, katika maisha ya hapa duniani nikichagua daima uzuri unaonielekeza katika furaha, nitakapokufa nitachagua furaha ya mbinguni. Nikiwa nimezoea kuchagua ubaya unaohatarisha uhai na utu, basi katika kifo pia nitachagua ubaya yaani motoni. Kweli mtu anaweza kuchagua kwenda motoni? Watu wanachaguaje ubaya katika maisha haya ya duniani, hata wakijua ni ubaya? Mara nyingi ubaya unaweza kuonekana kuwa unatuvutia; ubaya unaonesha njia ya mkato na unaonekana sawa tu! Labda maisha ya motoni pia yatakuwa hivyo – ya kutuvutia na kutuangamiza!