Vijana na Vyombo vya Mawasiliano

UTUME KWA VIJANA 8

Sahaya G. Selvam, SDB

Vijana na Vyombo vya Mawasiliano

Tupende tusipende nyakati hizi za karne ya 21 tumelazimika kutumia vyombo mbalimbali vya mawasiliano, kama vile, magazeti, simu, redio, kinasa sauti, runinga, video, mtandao, n.k. Vyombo hivi vimechangia katika kufanyia dunia yetu kuwa ndogo sana.  Vinachangia katika kuendeleza utandawazi, na katika usambazaji wa utamaduni wa kimagharibi.  Tunaweza kuvitumia vyombo hivi kwa ajili ya kujielimisha na kujiburudisha.  Maendeleo ya vyombo hivi yanatubabaisha.  Yaani, kila wakati vyombo hivi vinakuwa vya teknolojia mpya na vya rahisi kutumia.

 

Kwa vile, ni kawaida kwa vijana kuvutiwa na mambo mapya, hata maendeleo ya vyombo vya mawasiliano yanawashangaza sana. Vijana wanapenda pia kuunganika daima na vijana wenzao kwa njia ya kuvitumia vyombo hivi.  Kwa hiyo, wao huwa wanapenda kuzitumia aina mpya za vyombo vya mawasiliano, na pia kuvitumia sana.

 

Dunia ya mawasiliano inaweza kuchochea ubunifu wa vijana. Inaweza kuwasaidia kujielimisha na kujiburudisha. Aidha, inaweza kusababisha vijana kupoteza mali na muda mwingi.  Vilevile vyombo hivi vinachangia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko ya kiutamaduni hasa kati ya vijana.  Lakini uzuri au ubaya wake vyombo vya mawasiliano hutegemea na matumizi yake.

 

Katika makala hii tutazungumzia juu ya athari za matumizi ya vyombo vya mawasiliano, pamoja na kuangalia, katika utume kwa vijana, namna ya kuwasaidia vijana ili wasiathirike na matokeo mabaya ya vyombo vya mawasiliano, badala yake namna gani wanaweza kufaidika na matumizi ya vyombo hivi.

 

Vijana na Vyombo vya Mawasiliano Afrika Mashariki

 

Kadiri ya utafiti uliofanywa kati ya vijana wa nchi za Afrika Mashariki mambo haya muhimu yamegunduliwa:

  • Redio bado ni chombo kinachotumika sana kupita vyombo vingine vyote.  Kwa njia ya redio vijana wanapenda kusikiliza muziki ya wasanii wazalendo, na kwa vijana wa mijini wao hupenda pia wasanii wa nje.  Na kwa upande wa wasichana wao mara nyingi hupenda sana vipindi kama zile za “chombeza time” na “weekend show”. Programu hizi mara nyingi zinahusu urafiki na mapenzi.
  • Kwenye magazeti wavulana wanapenda kusoma habari za michezo, na wasichana wanapenda habari za wanamuziki. Kwa ujumla, vijana wanapenda sana kusoma sehemu za maswali na majibu, kama “Anti Liza”(Tanzania), na Amani Counselling (Kenya).
  • Simu za mikononi zinatumiwa zaidi na watu binafsi, kuliko simu za kawaida.  Simu za mikononi zimekuwa ishara ya kuenda na wakati, na mara nyingi kuwa na simu imekuwa tu maonyesho badala ya kutumika kwa haja za mawasiliano.
  • Aina za filamu za Nigeria zinapendelewa sana na vijana wa Afrika Mashariki.  Ingawa filamu hizi zinatumia lugha ya kiingereza, kwa vile waigizaji ni waafrika na mada zenyewe zinagusa maisha yetu ya kawaida, filamu za kinigeria zinawavutia wakazi wa Afrika Mashariki.  Hata hivyo, filamu hizi zinaonekana kuwa nzuri zaidi zikilinganishwa na zile za kimarekani.
  • Inasemekana kwamba wavulana walio wengi huwa wanapenda kuona filamu za mapigano, wakati wasichana wanapendelea zile za hadithi halisi.  Na kwa upande wa runinga, wavula wanapenda kuona programu za spoti, na wasichana wanapenda sana aina za tamthilia, na hasa zile zinazohusu mahusiano kati ya watu wa jinsia tofauti. Jambo la kushangaza ni kwamba, tamthilia za kiingereza zinaonekana kupendelewa zaidi kuliko zile za kiswahili.  Tamthilia kama vile Bold & Beautiful, Camilla, La Mujer de Lorenzo, zinasemekana kuwa zinaangaliwa sana na wasichana.
  • Kumbi za video zinawavutia vijana wengi hasa wa vijijini. Filamu za mapigano na mara nyingine hata za ngono (“Blue films”) zinaoneshwa kwa viingilio vya bei rahisi kwenye kumbi hizi zilizopo sehemu za vijiweni karibia kila kijijini. Utamaduni wa baa, pamoja na kumbi za video vinaendelea kuchangia katika kusambaza Virusi vya Ukimwi.
  • Mtandao bado ni chombo cha vijana wa mazingira ya mijini.  Tena, wanaotumia mtandao mara kwa mara ni wachache sana; vijana wengi, na hasa wale wa vijijini, wamewahi kutumia mtandao walau mara moja tu ili kufahamiana na chombo hiki.  Hivyo, wanaweza kujivunia kuwa wanatumia barua pepe, japokuwa anwani yao imeshafungwa. Hivyo basi tunaweza kusema kuwa watumiaji wengi wa mtandao hawajaelimika ipasavyo juu ya matumizi ya mtandao hasa katika nyanja za utafiti katika masomo, na badala yake umeishia tu kutumika kwa ajili ya “chatting” tu, pamoja na kuangalia picha za ngono.
  • Kwa ujumla, ingawa vyombo vyote vya mawasiliano vinaweza kutumika kwa ajili ya kujielimisha, vijana walio wengi wa Afrika Mashariki huwa wanavitumia kwa ajili ya kujiburudisha tu.  Kutokana na hali hii, inawapasa wazazi na walezi wa vijana kuwafundisha vijana namna ya kutumia vizuri vyombo vya habari, kuliko kuendelea kuvilaumu tu.

 

Athari za Matumizi ya Vyombo vya Mawasiliano

Lengo la makala hii si kuchoro picha hasi juu ya vyombo vya habari.  Vyombo hivi vina faida zake nyingi tu endapo vijana hawa wataweza kuvitumia kwa mpango mzuri.  Nadhani ni vyema basi, hapa kutaja athari walau chache za matumizi ya vyombo vya mawasiliano, hasa kati ya vijana.

  • Vyombo vya mawasiliano vimekuwa kama waalimu wa kisasa. Kwa vile vijana  wanashinda muda mwingi pamoja na vyombo hivi, vina uwezo mkubwa wa kuathiri fikra na tabia zao. Vyombo hivi vinaendelea kurusha mifano ya kuiga ambayo vijana wetu wanavutiwa kufuata.  Hivyo vijana wanaweza kujifunza taarifa mbalimbali kirahisi na kupanua akili zao, lakini pia wanaweza kujifunza mambo mabaya.
  • Programu za runinga kama zile za nchi za magharibi zinaleta utamaduni mpya.  Utamaduni huu ni wa kibepari, ni utamaduni wa mahusiano ya juu juu, na kwa ujumla niseme ni utamaduni wa maonyesho tu.  Vijana wa Afrika wanavutiwa kuiga utamaduni huo. Matangazo mengi ya biashara yanaonesha mazingira ambayo ni ya kigeni, na si ya kiafrika, hivyo hii huchangia katika kuchochea hamu ya kupata mali na starehe kwa njia za haraka haraka. Matangazo haya yanachochea mahitaji yasiyo ya lazima.  Ingawa hali hii inaweza kuwamotisha vijana kufanya kazi kwa bidii, lakini vilevile inaweza kuwashawishi kuwa na tabia ya kukusanya mali kwa njia zisizo halali.
  • Picha za ngono (pornography) zinazopatikana kirahisi katika mtandao na katika video zinawasukuma vijana wetu kutawaliwa na tabia mbaya za kimapenzi.  Hatimaye tabia hizi zinawalazimisha vijana kupoteza heshima kwa miili ya binadamu, hasa ya wanawake.
  • Licha ya athari ya kijamii na kimaadili, vyombo vya mawasiliano endapo havitatumika vizuri basi vinaweza kuleta matokeo ya ajabu.  Wataalamu wanasema kwamba watoto ambao hawajaanza kwenda shule wakiona picha za runinga (TV) uwezo wao wa kumsikiliza mwalimu darasa huwa unapunguwa.  Watoto daima wanatazamia vichokoo vinavyowavutia, wasipovipata wanakataa kujifunza.  Tusisahau kwamba wahudumu wa nyumbani (“house-maids”) mara nyingi huangalia TV wakiwa wameshika watoto!

 

Namna ya kuwasaidia Vijana katika Matumizi ya Vyombo vya Mawasiliano

 

Vyombo vya mawasiliano vyenyewe havina ubaya.  Ubaya wake ni kwamba hutokana na matumizi mabaya.  Kwa hiyo, kuwafundisha vijana kutumia vizuri vyombo vya mawasiliano ni sehemu muhimu katika utume kwa vijana.

1. Kuwapa vijana nafasi ya kupata ujuzi na taarifa kuhusu vyombo vya mawasiliano:

Tukijua teknolojia na siri za dunia ya vyombo vya mawasiliano tunaweza kwa kiasi kikubwa kupunguza athari zao juu ya fikra na tabia zetu.  Vijana wakipewa taarifa halisi kuhusu historia, teknolojia, lugha, urembo na mifumo ya vyombo mbalimbali vya mawasiliano vijana wanaweza kuvitumia kwa makini zaidi bila hata kuathirika na shikinizo zake.  Taarifa hizi zinaweza kutolewa kwa kupitia semina, warsha na mikutano.  Pia magazeti na matangazo ya ukutani yanaweza kutumika katika taasisi ya vijana.

 

Vijana wanatakiwa kutambua jumbe-siri za mawasiliano.  Hivi vyombo vya mawasiliano mara nyingi vina ujumbe uliofichika ambao unaziathiri akili za watazamaji.  Kwa mfano, matangazao mengi katika runinga yanaonesha familia ikitangaza bidhaa zao (kama dawa ya meno – Whitedent, or Coca-Cola, n.k.), familia hizi huwa ni zenye watoto wawili – mmoja wakiume na mwingine wakike.  Matangazo haya kwa nje yanatangaza bidha zao, lakini pia kwa siri zinasisitiza uzazi wa mpango.

 

Aidha, vijana wasisahau kwamba wanatoa ujumbe pia kwa kupitia nguo walizovaa na kwa lugha ya mwili.  Nguo zao ni vyombo vya mawasiliano.  Hivyo, yafaa wachague vizuri nguo zao.  Kwa mfano, wasivae T’shati zenye maneno ambayo wenyewe hawaelewi maana yake.  Vilevile, mitindo mbalimbali ya nguo inatoa ujumbe wake.

 

2. Kutoa changamoto kwa vijana kuwa watumiaji wamakini wa  vyombo vya mawasiliano:

Kwa kupitia ujuzi na taarifa kamili vijana wanaweza kusaidiwa kuwa watumiaji wamakini wa vyombo vya mawasiliano.  Watumie vyombo vya mawasiliano kwa ajili ya kujielimisha pia, si kwa ajili ya kujiburudisha tu.  Watumie vyombo hivi kulingana na shughuli zao nyingine.  Vijana wanahitaji kujifunza namna ya kutumia muda wao katika shughuli zao zote – kwa vile, masomo, sala, shughuli za nyumbani, kufahamiana na watu, michezo ya uwanjani.  Kujiburudisha katika mazingira ya nje ni muhimu pia!

 

Vijana wanahitaji kujifunza namna ya kutumia vyombo vingi iwezekanavyo kupata habari kamili. Kwa mfano, wakitumia TV tu, kupata habari za nchi, habari hizi zitakuwa zimechaguliwa kadiri ya chombo cha TV.  Wanaposoma pia magazeti wanaweza kupata habari kamili zaidi.

 

3. Kuwawezesha vijana kuchangia katika kuinjilisha mazingira ya vyombo vya mawasiliano:

Katika hati ile ya Sinodi ya Afrika – Kanisa Barani Afrika (1995), Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, anasisitiza kwamba, “Mazingira ya vyombo vya mawasiliano, ni zana nzuri katika utume wa kanisa kuiinjilisha dunia, vilevile mazingira ya vyombo vya mawasiliano yenyewe ni dunia inayohitaji kuinjilishwa.”  Kwa kusema hivi, anamaanisha kuwa, wakati tunaendelea kuvitumia vyombo vya mawasiliano katika shughuli zetu za kueneza injili, mazingira ya vyombo vya mawasiliano yenyewe yanatakiwa kusafishwa kutokana na dondoo zilizo kinyume na maadili ya kiinjili.

 

Katika wajibu huu wa kanisa vijana wana sehemu kubwa ya kuchangia.  Kwa hiyo, badala ya vijana kuwa wapokeaji wavivu katika dunia ya mawasiliano, wawe pia wanachangia katika kuboresha dunia hiyo.  Vijana wanahitaji kuwezeshwa kwa kupewa mbinu mbalimbali za kutoa changamoto kwa vyombo vya mawasiliano. Malezi kwa vijana yalenge kuwafundisha mbinu kama vile za kuwaandikia wahariri wa magazeti, kuandaa majadiliano juu ya sinema (Cine-forums), kutunga muziki na nyimbo zenye ujumbe wa Kikristu, vilevile kuchangia makala kwa magazeti, n.k.

 

Aidha, ni changamoto kubwa kwa vijana kuendelea kutumia vyombo vya mawasiliano vya kiasili.  Vyombo vya mawasiliano vya kiasili ni rahisi kutumia, vinashirikisha watu, havina mawazo ya kimagharibi, vinaleta mshindo-nyuma mara moja, na ni vya gharama ndogo.  Vinaweza kutumika kwa ubunifu hasa katika uinjilishaji.  Vyombo vya kiasili vinaweza kutumika pia kwa kupitia vyombo vya kisasa, k.m. kuleta michezo ya utamaduni katika runinga.  Vyombo vya mawasiliano vya kiasili daima vitakuwa vyombo mbadala wa vyombo vya kisasa.  Hivyo, tunaweza kukabili mawazo ya kibepari na ya kimagharibi.

 

(Itaendelea…)