Spoti na Utume kwa Vijana

UTUME KWA VIJANA 14

Sahaya G. Selvam, SDB

Spoti na Utume kwa Vijana

 

Ujana ni kipindi katika maisha ya binadamu chenye nguvu nyingi.  Spoti ni mkondo mzuri wa kutumia nguvu hii, na pia njia nzuri ya kujiburudisha kwa vijana.  Burudani ina sehemu yake muhimu katika maisha ya binadamu ili tuwe na afya ya kimwili na ya kiakili.  Ndiyo maana binadamu anaitwa homo ludens, yaani, binadamu mchezaji!  Anapotumia nguvu yake kwa ajili ya kutafuta riziki, hii ni kazi; lakini anapofanya mambo ya burudani na ubunifu bila kutafuta faida yoyote, huu ni mchezo.

 

Basi, katika makala hii ningependa kushirikisha nanyi mawazo machache kuhusu spoti na utume kwa vijana.  Yaani, jinsi michezo, hasa spoti, inaweza kutumika vizuri katika malezi ya vijana. (Michezo kwa ujumla inaweza kumaanisha hata ngoma na tamthilia, lakini spoti ni michezo inayofanyika uwanjani na kuwapa watu nafasi ya kukimbia na kuvinyosha viungo vya mwili.)  Michezo ni njia nzuri ya kuwavutia vijana katika mazingira ya kanisani.  Michezo inawapa nafasi nzuri siyo ya kustarehe tu bali ikitumika vizuri inaweza kusaidia kujenga tabia nzuri kati ya vijana.  Ndiyo maana watakatifu Filip Neri (1515-1595) na Johane Bosco (1815-1888) waliwahi kutumia michezo katika malezi ya vijana. Waliunganisha vizuri michezo na muziki, pamoja na, sala na mafundisho katika vituo vilivyoitwa “Oratori”. Vituo hivi vilikuwa na mafanikio makubwa katika malezi ya watu, hasa ya vijana.

 

 

Faida za Spoti kwa Vijana

 

Bila shaka spoti ikiwa inaongozwa vizuri ina faida nyingi kwa vijana:

  • Burudani: Spoti ni nafasi nzuri kwa vijana kujiburudisha bila kupoteza msimamo wa kimaadili, wala kujiingiza katika mazoea mabaya.  Katika spoti wanaweza kutumia vizuri muda uliobaki nje ya kazi au masomo.
  • Afya: Spoti hujenga afya.  Ujana ni kipindi cha mabadiliko ya kimaumbile, tena vijana wanapenda kujitunza kimwili. Pia wana nguvu ya ajabu. Spoti inaweza kuwapa fursa ya kujenga misuli na viungo, hivyo kupendeza na kujenga nguvu mwilini.  Kwa kutumia spoti, ambayo ni burudani halali, vijana hupunguza shinikizo la maisha, hivyo wanaweza kuwa na afya ya kiakili pia.
  • Stadi za maisha ya kijamii (Social Skills): Uwanja wa michezo ni sehemu nzuri ya kukutana na marafiki.  Hivyo, vijana wanapata nafasi ya kujenga stadi za kijamii.  Wanapocheza pamoja vijana huwa wanajifunza namna ya kupatana na watu, jinsi ya kuheshimiana, na hatimaye hupata njia za kufanikisha kazi katika vikundi. Wengine wanajifunza namna ya kuwa viongozi bora, na wote hupata fursa ya kujenga urafiki na uhusiano unaofaa.  Hata michezo ya kimataifa huunganisha watu wa makabila na lugha mbalimbali. Spoti halisi huonesha amani na umoja.
  • Kurekebisha tabia: Don Bosco aliwahi kusema kuwa kijana anapokuwa uwanjani hana kinyago, yaani, yu mwenyewe.  Anajisahau, na kuonesha tabia zake zote.  Kwa hiyo, mlezi akiwa uwanjani pamoja na vijana anapata fursa ya pekee kumwonya, kumkosoa, na hivyo kumlea kitabia.
  • Ajira: Spoti inaweza kuwapa vijana nafasi ya ajira. Endapo vijana watafundishwa vizuri michezo fulani, yaani, kama yuko kocha ambaye huwapa mazoezi kwa utaratibu na ufasaha, vijana wanaweza kuwa wachezaji katika timu za kitaifa na kimataifa, hivyo kupata pia riziki yao.

 

 

Hatari za Spoti katika Malezi ya Vijana

 

Pamoja na faida zilizotajwa hapo juu, endapo hakutakuwepo na mlezi mzuri, michezo inaweza kuwa njia ya kujenga msimamo potovu kati ya vijana.  Nitaje hatari chache katika malezi ya vijana kutokana na michezo isiyo na mwongozo:

 

Mifano mibaya ya wachezaji maarufu: Vijana huvutiwa na wachezaji maarufu.  Ni kawaida kwa vijana kukata picha za watu maarufu, hasa wachezaji na wanamuziki, na kuzibandika katika ukuta wa vyumba vyao.  Vilevile wanapenda kuvaa t-shirti zenye picha za watu maarufu.  Kwa vile vijana wana ndoto zao za maisha ya baadaye, watu maarufu wanaweza kuwa mifano ya kujipa moyo ili kuzifikia ndoto zile. Lakini kwa vile vijana wanapenda kuwaiga watu hawa maarufu, wakati mwingine wanaanza kuiga hata tabia zao mbaya. Tunajua kuwa siyo watu wote maarufu ni watakatifu!

 

Hatari ya kujenga tabia mbaya: Kutokana na hali hii ya kuiga, vilevile kutokana na mshinikizo wa rika katika timu zao, vijana wanaweza kushawishika kujiingiza katika tabia mbaya.  Mara nyingi tunaweza kuwakuta vijana walio wanaspoti wanajiingiza katika tabia potovu kama vile utumiaji wa madawa ya kulevya, kufanya ngono bila kuwajibika, na kupigana na wenzao kirahisi. Kwa hiyo, spoti peke yake haitaweza kuzizuia tabia mbaya. Lakini spoti inayoendana na malezi bora hujenga msimamo wa vijana.

 

Ubinafsi na ubepari: Siku hizi spoti imechukua sura ya biashara.  Wachezaji pamoja na mameneja wa spoti wanatafuta faida ya kiuchumi kutoka spoti.  Kutokana na hali hii, mashindano yanazidi,  na mara nyingine hata udanganyifu unaingia.  Wanaspoti wapo tayari hata kutojali utataratibu wa spoti mradi washinde na kupata tuzo.  Katika mazingira ya spoti kimataifa wanariadha wengine hutumia madawa ya kulevya ili wapate nguvu za ajabu. Wanaspoti wengine wanakula na kutoa rushwa ili kufanikisha timu fulani kwa faida ya washika dau (kwa kiingereza zoezi hili huitwa, “match fixing”).  Wengine hubadilisha uraia wao ili wapate nafasi nzuri pamoja na mshahara mzuri kutoka wajiri wao.  Hata washabiki katika uwanja wa kimataifa hukosa nidhamu na kuleta fujo na uharibifu (yaani, hooliganism). Kwa ujumla spoti imekuwa zoezi la ubepari, na wanaspoti hawasiti kufanya juu chini ili wapate faida katika biashara hiyo.

 

Dalili hizi zinaweza kuonekana  hata wakati wa spoti zinazoendeshwa katika mazingira ya kanisani.  Katika tamasha la vijana mara nyingi mechi inaweza kuishia katika mapigano; makocha wanaweza kubadilisha umri wa wachezaji ili timu zao zishinde; tena katika mechi kati ya vijana wakatoliki tunaweza kuwakuta wachezaji wa dini nyingine.  Mlezi mwenyewe anaweza kushawishika kuruhusu mambo haya kuhakikisha kuwa timu yake imeshinda. Roho ya ushindani inapozidi katika michezo kuliko roho ya spoti (sportsmanship) malengo halisi ya spoti yenyewe yanahatarishwa.

 

Kujiumiza kimwili: Wanaspoti wengi wana tabia ya kujisukuma kufanya mambo ambayo si kawaida kwa binadamu.  Wanajilazimisha kimwili mno mpaka wanatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha viungo vya mwili, kama vile magoti, mabega, kisigino, n.k.  Kwa hiyo, ingawa spoti inaweza kusaidia afya bora, roho ya ushindani inaweza kuleta madhara kwa afya.

 

 

Tahadhari za Kuhakikisha Malezi

 

Kwa ujumla ningependa kusisitiza kuwa spoti peke yake haina uhakika wa kubainisha malezi bora.  Pamoja na spoti vijana wanahitaji mambo yafuatayo ili kuhakikisha mazingira yatakayosaidia malezi bora kati ya vijana:

 

Mlezi awepo pamoja na vijana: Uwepo wa mlezi kati ya vijana unaweza kujenga mazingira ya malezi.  Vijana wanaokuja katika mazingira ya kanisani ili kucheza wasipewe tu mpira.  Kabla ya kutafuta vifaa vya michezo mhusika ahakikishe uwepo wa mlezi.  Hata Padre – mlezi wa vijana – anaweza kucheza au walau kuwepo pamoja na vijana.  Au awepo kocha au mtu mwingine mzima ambaye anaweza kuwafahamu vijana na kuwaelekeza katika maadili mema.  Uwepo wa mlezi kati ya vijana unafanana na uwepo wa Mungu kati ya viumbe vyake – si kama polisi kuwakamata wanapokosea, bali kama mchungaji anayewaongoza kondoo zake.  Mlezi awepo kati ya vijana, na kuwapa uhuru wa kutosha.

 

Michezo ifanyike kwa utaratibu: Utaratibu wa kujiandikisha katika timu uwepo.  Utaratibu wa kulinda nidhamu kati ya wachezaji uwekwe wazi; na vijana wakumbushwe mara kwa mara kuhusu utaratibu huo.  Wachezaji waunde chama cha mchezo kinachokubalika kati ya vyama vilivyopo katika parokia.  Kila chama kiwe na viongozi wao pamoja na mlezi wao.  Pamoja na kucheza vijana hawa wasaidie katika shughuli za kanisa.

 

Semina, warsha na liturjia: Kwa ajili ya wachezaji wa michezo mbalimbali katika mazingira ya kanisani kuwepo na semina za mara kwa mara. Semina hizi ziwe na lengo la kuwapa vijana stadi za maisha ya kikristu. Hata liturjia za pamoja kama wachezaji inaweza kuwapa vijana nafasi ya kutafakari na kupanga maisha yao kadiri ya mapenzi ya Mungu.  Vijana wanaokuja kucheza katika mazingira ya kanisani watambue kuwa michezo ni sehemu ya malezi ya kikristu.  Kwa hiyo, licha ya mchezo hata, semina, warsha, liturjia, na mafungo ya kiroho yanahitajika kwa ajili ya malezi yao.

 

Kufunga tafakari yetu katika makala hii nitoe muhtasari wake katika vipengele vifuatavyo:

  • Ni dhahiri kuwa, spoti ina nafasi yake muhimu katika maisha ya ujana.  Spoti inaweza pia kuwavutia vijana katika mazingira ya kanisani.
  • Lakini bila ufuatiliaji, michezo inaweza kuleta madhara kati ya vijana.
  • Kwa hiyo, kuwepo na taratibu za kuwalea vijana, kama vile kuwepo kwa mlezi, pamoja na kuongoza semina, liturjia na mafungo ya kiroho kwa wachezaji.

 

Itaendelea…