Maisha ya Kiroho – 2

UTUME KWA VIJANA 11

Sahaya G. Selvam, SDB

Vijana, Tunaitwa kuwa Watakatifu!

Maisha ya Kiroho Kwa Vijana – 2

 

Katika makala iliyotangulia tulieleza kuhusu maana ya maisha ya kiroho kwa vijana.  Hapo chini tungependa kueleza vipengele saba vinavyoweza kuwasaidia vijana katika safari yao ya kujikamilisha.  Katika kuandika makala hii nimesaidiwa na Prosper Dionis, ambaye ni kijana mtanzania.  Kwa namna nyingine anaeleza jinsi yeye mwenyewe anavyoishi maisha ya utakatifu.

 

1. Kuadhimisha Maisha kwa Furaha

 

Kuadhimisha maisha kwa furaha ni ile hali ya kutambua ubora wa maisha na kutoruhusu mahangaiko ya maisha kutukatisha tamaa.  Maisha ni zawadi ya pekee kutoka kwa Mungu.  Zawadi hii ni kwa ajili ya kulindwa, kukuzwa na kuadhimishwa.  Taabu za maisha wala mahangaiko ya kila siku hayapaswi kuwa vizuizi vya sisi kutofurahia maisha. Kuadhimisha maisha kwa furaha ni fikra niliyo nayo kwamba maisha ni zaidi ya magumu ninayokutana nayo kwa sasa.  Kuadhimisha maisha ni kupokea zawadi ya maisha kama yalivyo, pamoja na taabu na raha.  Kuadhimisha maisha ni kuendelea kubadili mambo ambayo yanaweza kubadilishwa katika maisha na mazingira yangu, na kukubali na yale ambayo siwezi kuyabadili.

 

Kuadhimisha maisha kwa furaha haimaanishi kuchekacheka daima au kutafuta njia ya kujifurahisha tu, ila ni hali ya ndani, yaani moyoni au nafsini mwangu. Utulivu wa ndani unaniwezesha kufanya shughuli zangu vizuri zaidi.  Ni uwezo wa kujipokea mwenyewe na kukubaliana na matokeo ya uamuzi wangu.

 

Watu wawili wanaweza kuwepo gerezani lakini wakachukulia hali hiyo katika mtazamo tofauti mmoja anaweza kupokea hali hiyo na kutumia miaka yake gerezani kama nafasi ya kujifunza na kujitambua zaidi kutokana na makosa aliyofanya.  Kwa hali hiyo anaweza kukomaa zaidi na kuwa mtu mpya, na zaidi anapata nafasi ya kuadhimisha maisha kwa furaha hata gerezani.  Mwingine anaweza kukataa tamaa au kulaumu wengine, na kuchoka na maisha.

 

2. Kutimiza Wajibu wa Kila Siku

 

Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika hotuba yake fupi baada ya kuchaguliwa Papa alisema: “Baada ya Baba Mtakatifu Mkuu Yohane Paulo II, makardinali wamenichagua mimi ili niwe mchapa kazi hodari katika shamba la Bwana!”  Kwa maneno mengine, amesema kuwa amechaguliwa kuwa Baba Mtakatifu ili kutimiza wajibu wake kama mwanakanisa.  Tunamaanisha nini tunaposema kutimiza wajibu wa kila siku ni sehemu ya maisha ya kiroho?  Ni hali ya kuwajibika kikamilifu na kutimiza majukumu ya kawaida ya kila siku. Kwa mfano, kama wewe ni mwanafunzi basi unasoma kwa bidii masomo yako; na kama upo nyumbani unajishughulisha na shughuli zote za pale nyumbani.  Na kama unafanya kazi za ofisini unafanya kwa uaminifu zaidi.

 

Kwa nini tunasisitiza juu ya kufanya kazi?  Kwa sababu, kazi inatusaidia kupata riziki yetu, vilevile inatupa nafasi ya kujenga uhusiano na binadamu wenzetu. Kazi inatupa maana ya maisha yetu.  Tunaendelea kuunganika na Mungu katika uumbaji kwa njia ya kazi. Hivyo kwa njia ya kutimiza wajibu wetu wa kila siku tunaendelea kuiboresha dunia na maisha ya kibinadamu.  Ndiyo maana kutimiza wajibu ni sehemu ya maisha ya kiroho hasa kwa vijana.

 

3. Kupokea Msalaba wa Maisha

 

Sisi wakristu hatuna budi kukumbuka kuwa ni kwa njia ya msalaba ndiyo tumeweza kukombolewa na Yesu. Tena kupitia maandiko matakatifu Yesu anatualika kwa kusema “mtu yeyote atakaye kunifuata ajitwike msalaba wake mwenyewe na kunifuata.” (Lk 9:23)

 

Basi, kila waridi una mwiba.  Tunaweza kujifunza nini kutoka msemo huu?  Kama tunapenda kuadhimisha maisha kwa furaha ni lazima daima tujitahidi kupokea mahangaiko ya maisha yetu.  Hakuna maisha yasiyo kuwa na mahangaiko na mara nyingi mahangaiko yanatupa nafasi ya kujikomaza zaidi ili kumudu maisha vizuri zaidi.  Pia tutambue kwamba kuna baadhi ya vitu au hali ambazo hatuwezi kubadili ila ni kwa njia ya kupokea hali hizo tunaweza kuhisi wepesi wake.  Kwa mfano tuchukulie kijana fulani haridhiki na rangi ya ngozi yake.  Ni dhahiri kuwa kijana huyu ataishi maisha ya kutojipenda daima kwa sababu hawezi kubadili rangi yake.  Kitakachomsaidia ni kujikubali jinsi alivyo.  Mambo mengine tusiyoweza kubadili ni kama hali ya hewa, wazazi wetu, kifo, makosa ya zamani.  Haya yote tunahitaji kupokea jinsi hali ilivyo.

 

Uzuri wa msalaba huu ni kwamba baadaye kuna tuzo, yaani taji la ushindi.  Kuna methali za kiswahili inayosema, “Baada ya dhiki ni faraja”, au “Mchumia juani hulia kivulini”.  Kwa kifupi ni kwamba kama kijana yeyote anataka kuishi maisha ya kweli na yenye msimamo lazima apokee msalaba wa maisha.

 

Kuna mifano michache tunayoweza kutumia:

1. Kijana anayeingia jando.  Katika mila na desturi za kiafrika kijana alitahiriwa bila sindano ya kupunguza maumivu (ganzi), ili kuonyesha kweli kijana huyu amekomaa na kuwa mtu mzima.  Uchungu/msalaba wa maumivu ulitumika kama ishara ya mpito kutoka utotoni kwenda utu uzima.  Hii ni sawa na kusema, “hakuna maumivu, hakuna ukuaji.”

 

2. Mwanamke Mjamzito.  Ukiwauliza wazazi wengi watakusimulia kuwa kipindi cha ujauzito hasa katika hali ya kujifungua kuna uchungu mkali.  Lakini cha ajabu ni kuwa wanawake wengi wanapenda kupitia uchungu huo hata mara nyingi.  Hii ni kwa sababu uchungu huu ni wa kitambo tu ingawa ni uchungu mkali, lakini furaha inayopatikana baadaye ni kuu kuliko uchungu huo.  Hii ni sawa na kusema, “hakuna maumivu, hakuna uhai.”

 

Ndiyo maana halisi ya kupokea msalaba katika maisha yetu ya kiroho.  Kijana yeyote anayeamua kuanza safari ya kujikamilisha awe tayari kupokea misalaba midogo midogo kama vile kuwa na msimamo katika vishawishi, pengine kuchekwa na wenzake kwa sababu ya msimamo wake, n.k.

 

4. Kuunganika na Mungu Kwa Sala

 

Sala ni sehemu muhimu wa maisha ya kiroho.  Lakini kusali hakuna maana ya kusema tu sala fulani, wakati uliopangiwa.  Bali ni kuunganika na Mungu daima.

 

Je, naweza kuunganika na Mungu daima?  Au naweza kusali daima?  Najua maswali haya yana majibu tofauti kwa watu tofauti.  Kwa ufupi ni kwamba upo uwezekano wa kuunganika na Mungu daima.  Kila unapotambua au kukumbuka uwepo wa Mungu kwa namna yoyote ile, umeunganika na Mungu.  Hata mahangaiko yako ya maisha yanaweza kuwa chanzo cha wewe kuunganika na Mungu.

 

Mungu anatamani tuungane naye kwa sala daima lakini sisi tunapotea katika kelele za dunia na kuzama katika shughuli zetu za kila siku, kiasi ambacho tunashindwa kumsikia Mungu anapotuita.  Mtakatifu Paulo anatuambia: “Salini daima.” (1The 5:17) Tutambua kwamba kusali sio ile hali ya kutumia sala rasmi tu; ila kuna mbinu nyingi za sala.  Sala ni kujituliza mbele ya uwepo wa Mungu.  Ninapojituliza ninatambua makosa yangu na kuonja neema ya utakaso.

 

5. Kutambua Maisha ni Wito na Utume

 

Katika mafundisho ya katekisimu ya awali tulifundishwa kuwa Mungu ametuumba ili tumjue, tumpende na tumtumikie.  Tunamjua Mungu kwa kutambua kuwa anatuita kufanya nini na tunaitikia wito wake.  Kila mmoja wetu ana wito fulani.  Kwa maneno mengine, Mungu anamhitaji kila mmoja wetu kufanya jambo fulani maalumu katika dunia hii.  Ni sehemu muhimu wa maisha ya kiroho kutambua mpango huo wa Mungu.

 

Tunapotambua mpango wa Mungu, yaani wito wetu, tunahitajika kuutimiza katika maisha yetu.  Ndio utume wa maisha. Kwa sisi vijana tunaweza kuwa wanachama wa vikundi mbalimbali vya uinjilishaji kwa wenzetu.  Na huu ni utume wa rika, yaani vijana kuwahudumia vijana wenzao.  Tunaweza kuwa na programu mbalimbali kama vila kuwatembelea wagonjwa, vituo vya watoto yatima, n.k. Pengine kusali tu kwa ajili ya wengine kunaweza kuwa utume.  Kwa njia hizi tunatambua kuwa maisha ni wito na utume kwa wengine.  Labda Mungu anakuita kwa wito maalum kama vile utawa au upadre. Tusisite kuitikia maana huko ni kujitoa zaidi kwa ajili ya wengi.

6. Ujihusishe na maisha ya kijamii na kisiasa

Mtakatifu si mtu anayetoroka kutoka jamii yake, wala anayeishi huko mawinguni.  Bali ni binadamu mwenye miguu yote miwili katika ardhi.  Yaani, maisha ya kiroho yanatualika kuishi kwa kina zaidi maisha ya dunia hii.  Mtakatifu ni mshiriki mkamilifu katika matukio mbalimbali ya mazingira yake.  Kipengele hiki kina maana ya pekee katika jamii ya kiafrika.  Hivyo, maisha ya kiroho yanakuwezesha kuchangia katika ustawi wa jamii na watu.

 

Kama vijana wakristu tunahitaji kujilea pia kujiingiza katika siasa ya nchi yetu.  Kweli siasa inahitaji kuinjilishwa.  Kazi hii haiwezi kufanyika kama wakristu wako nje ya siasa.  Ingawa mapadre na watawa hawawezi kuingia katika siasa kabisa, wanaweza kuwasaidia vijana katika wao kujilea kuwa viongozi.  Hivyo, tunaweza kujenga ufalme wa Mungu hapa duniani. Dalili za uwepo wa ufalme wa Mungu unatakiwa kuonekana katika kila kipengele cha jamii yetu.  Maisha ya kiroho ya kina yanatusaidia ili kuwasilisha ufalme huo katika kila pembe za dunia.

7. Uwe Mshiriki na Mjenzi wa Kanisa

 

Daima uwe sehemu ya Kanisa, kwa vile kanisa ndilo chombo cha pekee katika kukulea katika safari hii ya utakatifu. Kanisa linaweza kukusindikiza katika safari yako ya kiroho, kwa njia ya msaada wa jumuiya na sakramenti za kanisa.

 

Unaweza kuwa sehemu ya Kanisa kwa kujiunga na vikundi mbalimbali vilivyoko kanisani kama vile kwaya, watumishi, na vyama vya kitume pia kujitolea katika huduma ndogondogo kama kusafisha kanisa, kutunza mazingira, kupamba altare, nk.

 

Tunapoimarika zaidi tunaweza kuanzisha vikundi vya utume wa rika kwa ajili ya kuwainjilisha vijana wenzetu kwa kuwafikia mahali walipo mashuleni na katika vigango au parokia za jirani. Hayati Papa Yohane II wakati wa uhai wake alizoea daima kukiri kuwa vijana ni matumaini ya kanisa na daima alisisitiza tusiogope kuwa watakatifu wa milenia mpya. Sisi vijana tunanguvu za pekee hasa kwa kupitia vipaji mbalimbali tulivyo navyo. Kama tukiwa washiriki wazuri wa kanisa basi tutawainjilisha wengi zaidi kwa vipaji tulivyo navyo. Zaidi ya haya tutakuwa tunajiinjilisha wenyewe hatimaye kupata tuzo la utakatifu.

 

Kila mmoja wetu atambue kuwa kanisa ni sisi na sisi ni kanisa; kanisa bila wewe na mimi si kanisa. Hebu tujiulize swali hili: kama kijana unatumia vipi zawadi yako ya maisha katika kuwa mshiriki na mjenzi wa kanisa? Labda wengine tutajibu; “huwa naenda kanisani kila jumapili.” Wala hujakosea. Lakini hebu jaribu kujiuliza tena swali hili; unadhani kwa kwenda kanisani tu, umetumia vipaji vyako vyote? La hasha! Jibu liko wazi kabisa. Kanisa katoliki lina hazina kubwa kwa ajili ya vijana.

 

Mambo mengi katika maisha yanapatikana bure na moja ya hayo ni “Kuwa mshiriki wa Kanisa” ni bure kabisa na tuzo lake ni la juu kabisa, yaani “UTAKATIFU”

 

(Itaendelea…)

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *