Lectio Divina

UTUME KWA VIJANA 12

Sahaya G. Selvam, SDB

 

Lectio Divina Kwa Vijana

 

Tangu mwaka 1985, imekuwa desturi katika Kanisa Katoliki kuadhimisha Jumapili ya Matawi kuwa Siku ya Vijana Duniani. Aidha, kila mwaka katika adhimisho hili Baba Mtakatifu huwa anatoa ujumbe maalumu kwa ajili ya vijana duniani kote.  Hata mwaka huu wa 2006, katika adhimisho la 21 la Siku ya Vijana Duniani (9 April 2006), Baba Mtakatifu ametoa ujumbe kwa vijana wote: “Dhamira ninayopendekeza kwenu ni kutoka Zaburi 119: 105 –  “Neno lako ni taa ya kuniongoza, na mwanga katika njia yangu.”

 

Katika ujumbe wake anasisitizia kuwa vijana wa siku hizi tunaishi katika mazingira magumu yenye falsafa za uongo na maadili potofu.  Katika mazingira haya ya giza Neno la Mungu ndilo linaloweza kuiangaza njia yetu.

 

Papa anatukumbushia maneno ya mwandishi wa Waraka kwa Waebrania anayesema: “Neno la Mungu ni hai na lina nguvu; ni kali kuliko upanga wenye makali kuwili. Hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho hukutana, mpaka pale vikutanapo viungo vya mwili na mafuta. Neno hilo huchambua nia na fikra za mioyo ya watu” (4:12). Hivyo, hatuna budi kutumia Neno la Mungu kama “silaha-lazima” katika vita ya kiroho.

 

Baba Mtakatifu Benedikto XVI anatualika, “Vijana wangu wapendwa, tafakarini Neno la Mungu, na mumruhusu Roho Mtakatifu awe mwalimu wenu.”

 

“Njia moja ya kusoma na kuchambua Neno la Mungu iliyotumika muda mrefu”, Papa mwenyewe anatukumbushia,  “ni lectio divina, ambayo inaonyesha pia mfumo wa  safari ya kiroho iliyopangwa hatua kwa hatua.”

 

Katika makala hii ningependa kufafanua zaidi mbinu hii ya kutafakari Neno la Mungu na kuelekeza namna gani mbinu hii inaweza kutumika na vijana katika sala zao za binafsi hasa kwa njia ya kusoma Biblia.  Lectio Divina (maana yake halisi ni “Masomo ya kimungu”) ni njia ya kutafakari Neno la Mungu katika hatua nne.

 

Hatua ya Kwanza: Soma (Lectio)

Hatua hii ni kusoma na kurudia kwa uangalifu fungu la maandiko matakatifu na kutambua vipengele vyake mbalimbali.

  • Ujitulize mahali patulivu.  Jiweke kwenye hali ya kujituliza na uwe na nia ya kusali.  Pumua kwa makini mara chache ili kujituliza.
  • Umwombe Roho Mtakatifu kuwa pamoja nawe katika kipindi hiki cha sala. Unaweza kutumia sala au wimbo wa Roho Mtakatifu kwa lengo hilo.
  • Chagua fungu moja kutoka Agano Jipya, hasa kutoka katika Injili.
  • Soma fungu hili kwa taratibu sana, ukitambua kila neno.
  • Rudia kusoma mara nyingi kadiri unavyojisikia.  Usisome kwa lengo la kumalizia mistari mingi bali kwa ajili ya kutafuna Neno la Mungu katika fungu dogo.

 

Hatua ya Pili: Waza (Meditatio)

Hatua hii ni wakati wa kuwaza neno lile na kumgeukia Mungu kwa lengo la kuelewa Neno lake linatuambia nini leo.

  • Waza juu ya fungu ulilolisoma hasa ili kutambua lina maana gani kwako.
  • Rejea nafsini mwako sentensi yoyote inayokugusa. Unapojikuta umechoshwa na sentensi moja kutoka fungu lile, endelea na sentensi nyingine.
  • Maneno yanapokuchosha tulia na kutambua una fikra gani sasa hivi?  Fungu hili linachochea mawazo gani akilini mwake?
  • Usifikirie mno kiutaalamu bali kwa kutambua maana ya fungu hili kwa maisha yako leo.
  • Unapojisikia umeishiwa na mawazo ukae katika ukimya kwa kitambo kidogo kabla ya kuendelea na hatua inayofuata.

 

Hatua ya Tatu: Sali (Oratio)

Hatua inayofuata ni  oratio, ambapo tunazungumza na Mungu ana kwa ana.

  • Anza sasa kuzungumza na Mungu juu ya maana ya fungu hili.
  • Umruhusu Mungu pia kuongea nawe.
  • Jitahidi kukaa na fungu hilohilo… usianze kutoa maombi mbele ya Mungu kwa mahitaji yako mengi.  (Maombi ni njia moja tu ya kusali.  Lakini si njia inayofaa katika hatua hii.) Kusali ni kuwasiliana na Mungu.  Hivyo basi, katika hali ya unyenyekevu ongea na Mungu ukitumia fungu ulilosoma hapo awali.

 

Hatua ya Nne: Tafakari (Contemplatio)

Hatua hii inatusaidia kuuweka  moyo wetu tayari daima kutambua uwepo wa Kristu, kwa kuwa Neno lake ni “taa inayoangaza mahali penye giza mpaka siku ile itakapopambazuka na mwanga wa nyota ya asubuhi utakapong’ara mioyoni mwenu” (2Petro 1:19). Kusoma, kuwaza na kutafakari Neno kunatuwezesha kuishi maisha ya uaminifu kwa Yesu na kwa mafundisho yake.

  • Hatimaye jitahidi kutokufikiria wala kutumia neno lolote.
  • Kaa tu katika ukimya wa moyo wako.
  • Tambua hisia au vionjo vinavyotiririka moyoni mwako.
  • Umsikilize Mungu katika ukimya.
  • Katika hatua hii ya contemplatio, huangalii Neno la Mungu tena, lakini ukiongozwa na Neno lake unamwangalia Mungu mwenyewe.  Hutumii akili na fikra zako tena, bali unatumia moyo wako na hisia zako.  Huongei tena na Mungu, bali unamtazama tu katika ukimya, kwa kuwa Mungu ndiye mlengwa wa sala yetu.
  • Hatimaye unajiuliza, “Neno hili, fikra hizi pamoja na hisia hizi zina maana gani katika maisha yangu ya leo?”  Namna gani nitalitekeleza Neno hili katika maisha yangu.
  • Unapofunga kipindi hiki umshukuru Mungu kwa kuwepo kwake pamoja nawe muda huu wa sala, na katika maisha yako yote.

 

 

Hitimisho: Biblia katika Maisha ya Vijana

 

Siku hizi sehemu nyingi kuna mwamsho kati ya vijana kusoma Biblia.  Ingawa mtindo huu ni wa kusifika, sisi wakatoliki hatuna haja ya kuiga watu wa madhehebu mengine.  Biblia haikutungwa kwa lengo la kusoma na kubishana.  Bali lengo la Biblia ni ili tumjue Mungu na Mwanaye, na jinsi gani tuweze kujenga uhusiano wa karibu naye.  Mwalimu anapowaelekeza wanafunzi kuangalia mwezi angani, mwanafunzi mwenye busara huwa anaangalia mwezi, lakini mwanafunzi mpumbavu huwa anaangalia kidole tu.  Tukumbuke kuwa Biblia ni kidole kinachotuelekeza kwa Mungu.

 

Tushinde kila kishawishi cha kukariri mafungu kadhaa na kujivunia kuwa tumeijua Biblia.  Pia, tusiwe tunachambua sentensi moja moja bila kuelewa Neno la Mungu katika mazingira yake kwa ujumla.  Kuelewa Maandiko Matakatifu vizuri zaidi tunahitaji pia kujua historia ya Waisraeli, jiografia ya nchi takatifu na mazingira ya Yesu.  Biblia ni kama kiberiti ina nguvu ya kuwasha moto mkubwa; lakini katika mikono ya watu wasiojua matumizi yake inaweza kuleta uharibifu, na kuwapotosha watu.

 

Hatimaye, kujua Neno la Mungu ni kuishi Neno lile katika maisha yetu ya kila siku.  “Si yule atakayeniita, ‘Bwana, Bwana’, atakayeingia ufalme wa Mbinguni…” Tena, “Watu huutambua mti kutokana na matunda yake…. Mbona mwaniita ‘Bwana, Bwana,’ na huku hamtimizi yale ninayosema?” (Lk 6:44,46) Tusisahau kuwa hata ibilisi alikuwa amekariri Maandiko matakatifu na kuyatumia kwa ujanja katika kumshawishi Yesu mwenyewe (Lk 4:1-12; Mt 4:1-11).  Basi, kusoma Biblia kwenyewe hakuleti wokovu, bali kujenga uhusiano wa karibu na Yesu na Baba yake, na kuwapenda watu kama tunavyozipenda nafsi zetu.

 

Mbinu ya Lectio Divina inatusaidia kumkaribia Mungu kwa njia ya Neno lake lililohifadhiwa katika Biblia (hasa tunaposali na kutafakari Neno lake – oratio na contemplatio), na linaathiri fikra zetu na hatimaye linaingia katika matendo yetu (tunaposoma na kuwaza Neno lake – lectio na meditatio).

 

(Itaendelea…)