Familia na Vijana

UTUME KWA VIJANA 5

Sahaya G. Selvam, SDB

 

Kuwawezesha Vijana Kujenga Familia za Kikristu

 

“Kizazi hiki kimepotea. Vijana wa siku hizi hawana msimamo.  Kuna mmomonyoko wa maadili….” Haya ndiyo malalamiko tunayosikia kutoka kwa watu wazima.  Ukweli ni kwamba, tuwaleavyo vijana ndivyo wakuavyo! Hali ya vijana wa siku hizi ni matokeo ya hali ya familia zetu.  Na hali ya familia zetu si ya kujivunia.

 

Padre Shorter, mtaalamu wa mambo ya kijamii na kitamaduni, analalamika, “Katika jamii za Afrika siku hizi, mfumo wa familia umeathiriwa na mabadiliko ya kijamii na kimila.  Taratibu za jando na unyago zimeanza kupotea. Malezi kuhusu maisha ya kifamilia hayatolewi nyumbani wala shuleni.  Hivyo, vijana wamepoteza msimamo wao, nao kujiingiza katika mapenzi ovyo.” (African Culture: An Overview, 1998, p.95)

 

Mimi naamini kwamba ili kugeuza hali ya familia zetu kuna njia moja tu: inatubidi tuanze na vijana wetu.  Ingawa wengi wao wanatokea familia zilizobomoka, wanaweza kuzuia hali hii isiendelee zaidi.  Wanahitaji kuwezeshwa kuamua kujenga familia thabiti. Naamini kwamba, kuwawezesha vijana kujenga familia za Kikristu ni sehemu muhimu ya utume kwa vijana leo.  Katika makala hii ningependa kutaja dondoo chache zinazoweza kuwa msingi wa utume huo, wa kuwasindikiza vijana ili wazithamini familia za Kikristu, na kuwa na uwezo wa kujenga familia hizo. Dondoo hizi zinaweza kusisitizwa kwa kutumia mbinu nilizotaja katika makala iliyopita.

 

1. Maisha ya Ndoa ni Wito

 

Kila binadamu ana sehemu yake hapa duniani.  Ameumbwa na Mungu kwa ajili ya lengo la pekee. Kila mtu katika ujana wake anaalikwa kutambua nafasi aliyopangiwa na Mungu.  Hii ndiyo maana ya kutambua wito wetu.  Asipotimiza wito wake, hakuna mtu anayeweza kuridhika na maisha yake, wala kuwa na furaha ya kweli. Ni sehemu ya malezi ya vijana kuwasaidia kutambua wito wao.

 

Wengine kati ya vijana labda wanaitwa kujiunga na maisha ya utawa, na wengine kuwa mapadre.  Lakini wengi wao wanaitwa kuwa watu wa ndoa.  Maisha ya ndoa ni wito sawa na maisha ya utawa.  Kama ni wito, hata maisha ya ndoa yanapokelewa kwa heshima na uamuzi, pamoja na maandalizi ya kutosha.  Mtu haingii maisha ya ndoa kwa “bahati mbaya”!

 

2. Malengo ya Ndoa

 

Katika kuchagua au kutochagua wito wa ndoa vijana hawana budi kuzingatia malengo makuu ya maisha ya ndoa.  Tunaweza kutaja malengo makuu matatu ya ndoa : Upendo wa kina kati ya watu wawili wa jinsia tofauti, Kufurahishana kwa njia ya tendo la mapenzi, na Kuzaa watoto.

 

Malengo haya matatu yana umuhimu sawa katika ndoa.  Kuzidisha moja kuliko lingine kutaathiri mafanikio ya ndoa.  Labda utamaduni wa zamani wa kiafrika ulikuwa unasisitizia umuhimu wa uzazi katika ndoa. Utamaduni wa kisasa wa kimagharibi unazidisha umuhimu wa kufurahishana.  Bali ndoa ya kikristu inajengwa juu ya nguzo zote tatu.  Ukosefu wa kuelewa malengo ya ndoa katika vipengele vyote vitatu utaathiri maisha ya kifamilia.

 

3. Upendo wa Kweli una Subira

 

Kuna tofauti kubwa kati ya mvuto kati ya watu wa jinsia tofauti, na upendo kati yao.  Mvuto ni wa nje – ni wa umbo tu, lakini upendo ni wa ndani – ya moyo.  Mvuto unakuja kwa ghafla na kutoweka hivyo hivyo.  Upendo wa kweli ni uamuzi wa kuingia katika uhusiano ambao utawakuza wote wawili.  Mvuto unaelekea mapenzi ya mara moja.  Upendo wa kweli una subira. Vijana wanahitaji msaada mkubwa katika kutofautisha mvuto na upendo wa kweli.  Njia ya pekee ya kudhibitisha upendo wa kweli kati ya watu wawili ni kuona kama wapo tayari kuwajibika kuingia katika agano la ndoa kabla ya kuonja furaha ya mapenzi.

 

4. Mambo ya Mapenzi yana Sehemu yake katika Ndoa

 

Siku hizi kutokana na uwepo wa magonjwa kama UKIMWI, walezi wa vijana wanakishawishika kudai kwa ujumla kwamba mambo yote ya mapenzi ni dhambi, tena ni hatari.  Hili si fundisho zuri, wala si la kweli.  Vijana waoneshwe uzuri wa mapenzi, pamoja na heshima yake.  Mungu ametuumba ili tufikapo umri fulani tuwe na shauku ya mapenzi, ili tuweze kuonesha upendo wetu kwa mtu wa jinsia nyingine, hivyo kujifurahisha na kuzidisha vizazi vyetu. Kwa hiyo, tendo la mapenzi lina sehemu yake takatifu katika agano la ndoa.  Tendo la mapenzi linawagusa wale wanaojiingiza katika tendo hilo, kimwili, kihisia, kijamii, kiakili na kiroho.  Ndiyo maana, tendo hilo linatakiwa kulindwa katika boma la ndoa takatifu.

 

5. Uzazi wa kuwajibika ni Fundisho la Kanisa

 

Neno la Mungu kwa wazazi wa kwanza, “Zaeni muongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki” (Mwa 1:28), lilikuwa baraka si amri! Kwa hiyo upangaji wa uzazi (uzazi wa majira) si dhambi.  Bali, fundisho la kanisa linasisitiza uzazi wa kuwajibika. Ila kanisa linawaonya waumini wake juu ya baadhi ya mbinu za kisasa za kupanga uzazi.

Hati ya Baba Mtakatifu Paulo VI, Humanae Vitae inaeleweka wazi:

Upendo katika ndoa unawalazimisha wanandoa kutambua utume wao wa kuwa wazazi wanaowajibika….

Baada ya kutathmini mazingira yao ya kimaumbile, ya kiuchumi, ya kisaikolojia na ya kijamii, wazazi wenye watoto wengi pia wanawajibika.  Aidha, kwa sababu maalumu, wakifuata kanuni za maadili mema, wazazi wanaoamua wasizae watoto, kwa muda mfupi au hata kwa muda mrefu, pia wanawajibika. (na.10)

Hati hii inaendelea kusisitiza kwamba tendo la ndoa daima lifanyike kwa heshima na “inavyostahili hadhi ya utu” (na.11).   Vijana wetu basi waambiwe ukweli. Waelewe namna ya kuwa wazazi wawajibikaji.

 

 

 

6. Agano la Ndoa ni Muhimu kuliko Sherehe ya Harusi

 

Idadi ya vijana wakristu wanaojiingiza katika “ndoa za mkeka”, (au kwa kiingereza, come & stay marriages) inaongezeka siku hadi siku.  Sababu mojawapo ya hali hii ni vijana kushindwa kutoa mahari iliyopangwa na baba mkwe.  Pia wengine wanaogopa kujitolea kabisa katika uhusiano wa kudumu.  Lakini vijana wengi wakristu wanaishi katika hali ya ndoa bila sakramenti ya ndoa kwa sababu wanahofia gharama za kuandaa sherehe za harusi.  Vijana wanatakiwa kuelewa kwamba uthibitisho wa agano la ndoa kwa njia ya sakramenti ya ndoa ni muhimu zaidi kuliko sherehe ya harusi.  Watu wanaohitajika kwa ajili ya adhimisho la sakramenti ya ndoa ni wanandoa, mhudumu wa kanisa, na mashahidi wawili.

 

Parokia nyingi zina taratibu za kuwa na sherehe za harusi kwa watu wengi mara moja.  Nadhani hii ni njia nzuri ya kuwahamasisha watu kubariki ndoa zao. Aidha, ndoa hizi kanisani ni nafasi nzuri kutoa mafundisho kwa wanaojiandaa, kuhusu maisha ya kifamilia.

 

7. Wanaume na Wanawake wana Wajibu Sawa katika Familia

 

Uzuri wa mojawapo ya mabadiliko katika maisha ya ndoa ni kwamba mume na mke wameanza kukiri usawa wao. Ni lazima usawa huu uelekee wajibu si haki tu.  Pia usawa hauna maana kwamba yote yanayofanyiwa na wanaume yafanywe na wanawake.  Usawa kati ya watu unaheshimu tofauti za kimaumbile, za kitabia na za kiwajibu.  Kukosa heshima hii husababisha mmomonyoko wa familia zetu.  Usawa kati ya watu wa ndoa utaonekana katika uamuzi na mawasiliano katika familia.  Vijana wetu wanahitaji nafasi za kujikuza katika stadi za maisha, kama vile, namna ya kuwaheshimu watu wa jinsia tofauti, namna ya kufikia suluhisho la tatizo fulani kwa njia ya majadiliano, pamoja na mbinu za mawasiliano kinifu.

 

8. Watoto huhitaji Mazingira mazuri ya kifamilia ili Kujikamilisha

 

Watalaamu wa elimu ya binadamu (wana anthropolojia) huwa wanakiri kwamba kati ya makabila yote ya kiasili kuna taratibu maalumu za kuanza maisha ya ndoa.  Utaratibu huu ambao unadhihirisha mpango wa Mungu, ni kwamba vijana wawili wa jinsia tofauti wanaanza kufahamiana wenyewe kwa wenyewe, au wanasaidiwa na wazazi wao kufahamiana, halafu baada ya ibada au tukio maalumu wanaanza kuishi pamoja kama watu wa ndoa.  Na hatimaye wanakaribisha watoto ndani ya familia yao.

 

Watoto wa binadamu wanapozaliwa ni wadhaifu kuliko watoto wa wanyama wote.  Ndama anaweza kusimama na kurukaruka nusu saa tu baada ya kuzaliwa kwake.  Vifaranga vya bata vinaweza kuogelea siku hiyohiyo vilipoanguliwa.  Lakini mtoto wa binadamu licha ya kuwategemea wazazi wake kwa mahitaji yake yote kwa miaka mingi, anaweza kujitambua kiakili na kiroho kwa msaada wa binadamu wenzake tu.  Ndiyo maana watoto huhitaji mazingira mazuri ya kifamilia ili kujikamilisha.

 

9. Vijana Wazithamini Desturi za Kiafrika

 

Watumiaji wengi wa vyombo vya mawasiliano vya kisasa ni vijana.  Programu nyingine zinazorushwa katika vyombo hivi ni zile zinazotoa mifano potofu ya familia za jamii za kimagharibi.  Familia za aina hii ni za ndoto tu, na haziwezi kuleta maendeleo halisi kwa binadamu.

 

Vijana wetu wanahitaji pia mazoezi katika utumiaji wa vyombo vya mawasiliano ili wasiwe watumwa wa mambo potofu ya magharibi.  Ni lazima wasaidiwe kuzithamini desturi na mila za kiafrika zinazokuza utu.  Maendeleo halisi si kuwaiga wengine, bali ni kudumisha jamii yetu. (Tutazungumza zaidi kuhusu vyombo vya mawasiliano katika makala ya sita ya mfululizo huu.)

 

10. Kristu Ndiye Kichwa Halisi cha Familia za Kikristu

 

Askofu Fulton Sheen wa Marekani ameandika kitabu kimoja kinachohusu maisha ya ndoa, na kichwa chake cha habari ni “Watu Watatu Kuoana”!  Anamaanisha kwamba nafsi ya tatu katika ndoa za kikristu ni Kristu mwenyewe.  Ndiyo, wakristu wanaoana katika Kristu.  Maana yake ni kwamba familia za kikristu si taasisi za kijamii tu, bali zinajengwa juu ya imani.  Matatizo na kukosa mawasiliano katika ndoa ni kawaida tu lakini kuvumilia matatizo haya wanandoa wanahitaji imani. Mafanikio ya kiuchumi au watoto peke yao hawaleti furaha katika ndoa.  Bali, ni imani kwamba mwenzangu ni zawadi kutoka kwa Mungu ndiyo inayoweza kuwasaidia wanandoa kuwa na uaminifu katika ndoa.

 

Vijana hawawezi kuelewa vipengele hivi vyote kutokana na mahubiri tu.  Walezi wa vijana wanahitaji kuwa na ubunifu wa kutumia mbinu shirikishi ambazo nilizitaja katika makala iliyopita katika mfululizo huu. Mbinu zinazochochea majadiliano ndizo zinazoweza kujenga msimamo kati ya vijana juu familia za kikristu.  Zaidi ya mbinu bunifu, mfano hai uliotolewa na walezi kwa njia ya maisha yao wenyewe, unaweza kuleta mafanikio makubwa.

 

Familia ni chembechembe hai za jamii.  Familia ni kanisa dogo.  Kujenga kanisa kwa njia ya kujenga familia za kikristu ni sehemu muhimu katika utume kwa vijana.

 

(Itaendelea…)